Jun 12, 2021 13:06 UTC
  • Sayyid Abbas Araqchi
    Sayyid Abbas Araqchi

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Anayehusika na Masuala ya Kisiasa amesema ni kinaya kuiona Marekani inalia machozi ya mamba katika hali ambayo Washington inaendeleza jitihada zake za kuwataabisha na kuwahangaisha kwa njaa na umaskini Wairani milioni 82.

Sayyid Abbas Araqchi amesema hayo leo katika ujumbe aliotuma kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter na kuongeza kuwa: "(Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump) ameondoka, lakini vikwazo vyake vya kikatili na vilivyo kinyume cha sheria vingalipo."

Araqchi ameishangaa Washington kutaka kuionesha dunia kwamba ina huruma na mapenzi na wananchi wa Iran katika hali ambayo, nchi hiyo inaendelea kulisakama taifa hili kwa vikwazo na mashinikizo ya kiwango cha juu.

Mwanadiplomasia huyo anayeongoza timu ya mazungumzo ya nyuklia huko Vienna amebainisha kuwa: "Ugaidi wa kiuchumi katika kipindi cha janga la corona ni jinai dhidi ya binadamu."

Wakati huohuo, Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran Katika Umoja wa Mataifa ameukosoa vikali utawala wa Joe Biden wa Marekani, kwa kudeleza sera za Trump za ugaidi wa kiuchumi dhidi ya wananchi wa Iran.

Takht-Ravanchi

Majid Takht-Ravanchi alisema hayo jana Ijumaa kwenye kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na kusisitiza kuwa, madai ya Marekani kuwa imebadili sera zake mkabala wa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA yapo tu katika makaratasi, na kwamba wananchi wa Iran wangali wanahangaika kuagiza dawa kutoka nje ya nchi kutokana na kampeni ya ugaidi wa kiuchumi dhidi ya Tehran.

Duru mpya ya mazungumzo ya nyuklia kati ya Iran na kundi la 4+1 huko Vienna Austria inaanza leo Jumamosi. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inasisitiza kuwa itarejea katika kutekeleza kikamilifu majukumu yake kwa mujibu wa mapatano ya JCPOA pale Marekani itakapoondoa vikwazo vyote dhidi yake; na Iran pia kufanya uchunguzi na kuhakikisha ni kweli vikwazo hivyo vimeondolewa kikamilifu.

Tags