Jun 12, 2021 13:51 UTC
  • Njama za Saudia za kuzusha machafuko nchini Iran katika kipindi cha uchaguzi wa rais

Baada ya kupasishwa majina ya wagombea urais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, vyombo vya habari vya nchi hasimu za kanda ya Magharibi mwa Asia hususan vile vyenye mfungmano na Saudi Arabia na Imarati vilianzisha kampeni maalumu kwa shabaha ya kuwashawishi wananchi wasishiriki katika zoezi hilo na kuibua machafufuko hapa nchini.

Vyombo hivyo vya habari vimekuwa vikitumia mbinu na njia mbalimbali kutimiza lengo hilo ikiwa ni pamoja na kudunisha cheo cha Rais wa Jamhuri nchini Iran au kutoa madai kwamba, kushiriki wananchi katika zoezi hilo hakuna faida, na vilevile kutaka kuonesha sura isiyo sahihi kuhusiana na hali ya kisiasa ya sasa hapa nchini. Habari, ripoti, filamu na mahojiano yanayofanywa na vyombo hivyo na habari na waalikwa makhsusi na kuwekwa katika kurasa za mitandao ya kijamii, vyote vimejikita katika kuonyesha sura hasi na iliyopinduliwa kuhusu hali ya kisiasa ndani ya Iran ya Kiislamu.

Filamu fupi zinazorushwa hewani na Saudi Arabia kupitia mitandao ya kijamii ambazo kimsingi zinawalenga watu wa ndani ya Saudia kwenyewe, zina lengo la kufikisha ujumbe unaodai kwamba, chaguzi zinazofanyika katika Jamhuri ya Kiislamu ni za kijuujuu na kimaonyesho tu. Propaganda hiyo ya sura iliyopinduliwa na kupotoshwa kuhusu zoezi la uchaguzi wa rais nchini Iran inawalenga zaidi wananchi katika nchi za kidikteta za Ghuba ya Uajemi ili kulinda na kutetea kwa njia isiyo ya moja kwa moja tawala za kifalme na kidikteta katika nchi hizo. Hii ni kwa sababu, kufanyika chaguzi mbalimbali nchini Iran daima limekuwa kero kwa watawala madikteta wa nchi hizo za Kifalme wanaohojiwa na kushambuliwa na watu katika mitandao ya kijamii wakitakiwa kuwa na tawala za kidemokrasia na zilizochaguliwa na wananchi kama ilivyo Iran. Kwa mfano tu, katika siku hizi watumiaji wa mitandao ya kijamii wamekuwa wakiipiga vijembe Saudi Arabia na kuifanyia maskhara wakisema viongozi wa nchi hiyo wanakosoa anga ya uchaguzi nchini Iran ilhali uchaguzi wa mwisho ulifanyika Hijaz (Saudi Arabia) wakati makabila ya Waarabu yalipopiga kura kwa ajili ya kukubaliana juu ya namna ya kumuua Mtume Muhammad (saw).

Kwa msingi huo, ni jambo linaloeleweka kuona vyombo vya habari vya nchi kama Saudi Arabia na viongozi wa nchi hiyo vikishambulia na kutaka kuonyesha anga hasi kuhusiana na uchaguzi wa rais nchini Iran. 

Sambamba na hayo, vyombo vya habari vinavyomilikiwa na watu wa karibu na watawala wa Kifalme wa Saudia siku hizi vimejikita zaidi katika kuharibu sifa na hadhi ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu vikidai kuwa, rais wa nchi nchini Iran hana mamlaka ya kutosha. Ni wazi kuwa, propaganda kama hizi ni aina fulani ya jitihada za kutaka kufunika mfumo wa kidikteta unaotawala Saudia kupitia nja ya kuchafua mfumo wa utawala katika nchi hasimu. Vyombo hivyo vya habari pia vinaendeleza ajenda ya kutaka kuwavunja moyo wananchi wa Iran na kuwashawishi wasishiriki katika uchaguzi ujao wa rais na hatimaye kuzusha machafuko na vurugu kabla au wakati wa uchaguzi wa rais kupitia njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na kurusha hewani au katika mitandao yao ya kijamii picha na filamu zinazowaonyesha baadhi ya wagombea urais wakiwashambulia wenzao katika midahalo na kampeni za uchaguzi na kadhalika.

Ukweli ni kwamba, tangu baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, kwa wastani Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikiitisha uchaguzi kila mwaka katika kipindi chote cha zaidi ya miaka 42 iliyopita suala ambalo ni kilelezo cha mfumo unaotawala hapa nchini yaani demokrasia ya kidini. Suala hilo liliashiriwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei katika hotuba yeke kwenye kumbukumbu ya siku ya kuaga dunia hayati Imam Ruhullah Khomeini mapema mwezi huu. 

Ayatullah Khamenei aliashiria maendeleo na ustawi endelevu unaoshuhudiwa hapa nchini na kusema: Siri ya kubakia hai mfumo wa Imam Khomeini ni kuendelea kushikamana kwa mambo mawili yaani Jamhuri (wananchi) na Uislamu. 

Kiongozi Muadhamu ameongeza kuwa, miongoni mwa kazi kubwa zilizofanywa na Imam Khomeini ni kubuni fikra ya Jamhuri ya Kiislamu na kuingiza fikra hiyo katika nadharia za kisiasa za kimataifa na hatimaye kutekeleza nadharia hiyo kivitendo.

Amefafanua zaidi kwa kusema kuwa maneno mawili ya "Jamhuri"  na "Kiislamu" kwa maana ya utawala wa Uislamu na wananchi, ndio ufunguo wa matatizo yote.