Jun 13, 2021 15:09 UTC
  • Mdahalo wa tatu wa urais wa Iran, wagombea waeleza mipango yao na kukosoa mitazamo na utendajikazi

Mdahalo wa tatu na wa mwisho wa uchaguzi wa rais wa awamu ya 13 wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ulifanyika Jumamosi alasiri.

Madukuduku ya wananchi ndiyo iliyokuwa mada  kuu ya mdahalo huo ambao ulirushwa mubasahara na Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Katika mdahalo huo  wagombea  saba wa urais walijadili masuala mbalimbali ya kiuchumi, kijamii, na sera za kigeni. Maswali ya mdahalo huo yalikuwa yamepangwa kwa njia ambayo wagombea walitakiwa kueleza mipango yao na njia wanazopendekeza za utatuzi wa changamoto zilizopo.

Wagombea wote walionekana kusistiza haja ya kutumiwa uwezo wa ndani ya nchi huku wakieleza mipango yao kuhusu masuala kama vile ya ajira ya vijana, makazi bora na ya bei nafuu, mfumuko wa bei, ustawi wa soko la hisa, sekta ya afya na sera za kigeni.

Mdahalo huo ulikuwa fursa nzuri, ingawa ni kweli kuwa haiwezekani kuwasilisha mipango ya kutatua matatizo au madukuduku ya wananchi katika mdahalo wa masaa matatu. Hii ni kweli hasa kwa kuzingatia kuwa, kawaida katika midahalo kama hii baadhi wa wagombea huondoka katika mada na kujikita katika kuwakosoa wagombea wengine na utendaji wa serikali iliyoko madarakani.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Utoaji nara, tuhuma na kukosoa utendaji wa serikali ni nukta zilizojitokeza katika midahalo mitatu ya urais wa Iran mwaka huu. Tab'an, mbali na hayo kila mgombea ametoa ahadi tele kwa ajili ya kuwavutia wapiga kura.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu hivi karibuni katika hotuba yake aliwashauri wagombea wajiepushe na kutoa ahadi ambazo hawana uhakika wanaweza kuzitekeleza. Vilevile aliwataka wagombea wajiepushe na kubadilisha uchaguzi kuwa 'medani ya vita vya kuwaia madaraka na makabiliano ya kuvunjiana heshima' kama inavyoshuhudiwa katika uchaguzi wa Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya. Aliongeza kuwa, "Huko nyuma pia nchi ndiyo iliyopata madhara wakati midahalo na kampeni ziligubikwa na hali ya kuharibiana majina, tuhuma na kuwatisha wananchi kuhusu wagombea wengine."

Kilichowazi ni kuwa, utatuzi wa matatizo na kimasiha na ya kiuchumi, kupambana na ufisadi pamoja na ubaguzi ni kati ya matakwa ya kimsingi ya wananchi. Nukta hizo haziwezi kutatuliwa kwa ahadi tu. Ni wazi kuwa kujifunza kutokana na yaliyopita, kutegemea uwezo wa ndani ya nchi na kutumia watendaji wenye kufanya kazi kwa njia sahihi, kuimarisha uzalishji wa ndani, ustawi na kulinda mshikamano wa kitaifa ni kati ya mambo ya dharura katika kutatua matatizo yaliyopota.

Pamoja na hayo haipaswi kupuuza au kudunisha mafanikio ya serikali inayoondoka ambayo ilikuwa inakabiliana na hali ngumu ya vikwazo na janga la corona.

Nukta nyingine ni kuwa, haipaswi kupoteza matumaini kutokana na matatizo yaliyopita, bali kuna ulazima wa kukubali kwamba, kuna udhaifu na mapungufu, na baada ya hapo kutafuta njia za kutatua matatizo hayo kivitendo.

Mipango ya kiuchumi iliyowasilishwa na wagombea inaonekana kuwa imara, lakini inabidi itekelezwe kivitendo ili ubora wake ubainike. Pamoja na hayo ni ishara nzuri kuwa wagombea wote wamezingatia masuala ya kimsingi ya jamii hasa utatuzi wa matatizo ya vijana na kutumia vizuri uwezo wa ndani ya nchi katika kuimarisha sekta ya uzalishaji.

Wagombea urais wa Iran

Uchumi ni sekta pana sana na hivyo mdahalo wa televisheni hautoshi  kujibu madukuduku yote ya wananchi. Hivyo katika siku chache zilizobakia kabla ya uchaguzi wa Ijumaa, wagombea watakuwa na fursa ya kutosha ya kueleza vyema zaidi mipango yao na kujibu maswali yote ya wananchi.

Kwa ujumla ni kuwa, wagombea wate wa urais nchini Iran wanaamini kuwa, kuna ulazima wa kutegemea uwezo wa ndani ya nchi katika kuleta maendeleo sambamba na kulinda hadhi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hasa katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA na sera za kigeni.

Pamoja na hayo,  hali ya sasa ya nchi inahitaji kuchaguliwa mwanasiasa ambaye ana historia nzuri ya utendaji na uongozi wenye nguvu. Wananchi wa Iran wameonyesha kuwa, watashiriki kwa wingi katika uchaguzi ujao, na midahalo hii inawapa fursa ya kubaini mipango na mitazamo ya wagombea.

Tags