Jun 14, 2021 13:07 UTC
  • Ujumbe wa Kenya watembelea sekta ya teknolojia nchini Iran

Ujumbe wa ngazi za juu wa wadau wa sekta ya sayansi na teknolojia nchini Kenya uko safarini katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa lengo la kuimarisha uhusiano wa n chi mbili katika sekta hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ofisi ya Makamu wa Rais wa Iran anayesimamia masuala ya sayansi  na teknolojia katika safari hiyo ya siku saba ambayo imeanza Jumapili, ujumbe huo utakutana na kufanya mazungumzo na wawakilishi wa mashirika  ya sekta ya sayansi na teknolojia nchini Iran mbali na kutembelea mashirika kadhaa. Mazungumzo baina ya ujumbe wa Kenya na wenzao wa Iran yatahusu ununuzi wa bidhaa na huduma baina ya pande mbili. Halikadhalika mazungumzo hayo yanajikita katika uwekezaji wa sekta za mashine na bidhaa za kilimo.

Ikumbukwe kuwa  mwezi Januari mwaka huu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesema kuzinduliwa Kituo cha Ubunifu na Teknolojia cha Iran (IHIT) katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi kumefungua ukurasa mpya wa ushirikiano wa kiuchumi baina ya Iran na Kenya na hata nchi nyingine za kanda ya Afrika Mashariki.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo iliyofanyika mjini Nairobi, Makamu wa Rais wa Iran anayeshughulikia masuala ya sayansi na teknolojia, Dakta Sorena Sattari amesema Jamhuri ya Kiislamu inaunga mkono kikamilifu ushirikiano baina ya Nairobi na Tehran katika uga wa teknolojia.

Wawakilishi wa mashirika 40 ya kiteknolojia ya Iran katika nyuga za petrokemikali, nishati jadidika, utengenezaji dawa, bioteknolojia na nanoteknolojia walishiriki uzinduzi huo pia na kukutana na wafanyabiashara na wawekezaji wa Kenya.

Safari ya sasa nchini Iran ya ujumbe huo wa wawakilishi wa sekta ya teknolojia kutoka Kenya ni katika utekelezaji wa mapatano yaliyofikiwa katika safari ya Dkt. Sattari nchini Kenya.