Jun 14, 2021 13:08 UTC
  • Chanjo ya COVID-19 ya Iran ya COV-Iran Barekat yapata idhini ya matumizi ya dharura

Wizara ya Afya ya Jamhuri ya .Kiislamu ya Iran imetoa idhini ya matumizi ya dharura ya chanjo ya COVID-19 iliyoundwa hapa nchini ya COV-Iran Barekat

Waziri wa Afya wa Iran Daktari Saeed Namaki amesema Jumatatu kuwa: "Leo idhini ya matumizi ya dharura ya COV-Iran Barekat imetolewa na wiki ijayo pia  chanjo ya COVID-19 iliyoundwa na taasisi ya Pasteur ya Iran nayo itapata idhini."

Amesema kwa mujibu wa mipango iliyopo watu wote wanaolengwa nchini Iran wataweza kupata chanjo ya COVID-19 katika kipindi cha miezi sita ijayo.

 Dkt. Hassan Jalili  mkuu wa timu ya utengenezaji chanjo hiyo ya COV-Iran Barekat katika Idara ya Utafiti ya Taasisi ya Utekelezaji wa Maagizo ya Imam Khomeini (MA) alisema hivi karibuni kuwa tayari wameshazalisha dozi milioni moja za chanjo hiyo ambayo awamu yake ya tatu ya majaribio imekamilika. Alisema dozi hizo zitakabidhiwa Wizara ya Afya kwa ajili ya kusambazwa nchini.  Amesema hivi karibuni hivi wanatarajia kuzalisha dozi milioni 18 za chanjo ya COV-Iran Barekat.

Mwanadamu wa kwanza kupigwa chanjo ya majaribio ya corona nchini Iran

Iran iko mstari ya mbele kuunda chanjo za COVID-19 ambapo mbali na  chanjo ya  COV Iran Barakat , chanjo zingine ambazo zimepiga hatua nzuri katika majaribio ni pamoja na Razi Cov Pars,  Fakhra na chanjo ya pamoja ya Taasisi ya Chanjo ya Finlay ya Cuba na Taasisi ya Chanjo ya Pasteur ya Iran.