Jun 17, 2021 08:37 UTC
  • Mtazamo wa Kiongozi Muadhamu kuhusu umuhimu wa kushiriki kwa wingi wananchi katika uchaguzi wa rais

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzui ya Kiislamu Ayatullah Khamenei amesema kuwa, kushiriki wananchi kwenye maamuzi ya kitaifa kwenye mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ni msingi na nguzo muhimu ya kifikra na wala si suala la kisiasa tu.

Amesema japokuwa kushiriki huko kwa wananchi kuna faida nyingi za kisiasa lakini muhimu zaidi ni falsafa ya kushirikishwa wananchi katika masuala ya utawala kwenye mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, kwa maana kwamba, katika Jamhuri ya Kiislamu kuna "Jamhuri" yaani watu, na "Uislamu"; na iwapo wananchi hawatashirikishwa basi Jamhuri ya Kiislamu haitakamilika. 

Ayatullah Ali Khamenei aliyasema hayo alasiri ya jana katika hotuba yake kwa taifa na kuongeza kuwa Rais wa Jamhuri atakayechaguliwa siku ya Ijumaa, iwapo atachaguliwa kwa kura nyingi atakuwa rais imara na madhubuti, na ataweza kufanya kazi kubwa zaidi.

Ayatullah Khamenei

Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu na fikra za Imam Ruhullah Khomeini, uchaguzi ndiyo njia ya kutekeleza demokrasia katika mfumo wa demokrasia ya kidini wa Iran, na ni nguzo muhimu katika utawala wa sasa wa Iran. Uchaguzi ukilinganishwa na masuala mengine, una nafasi muhimu sana katika kuzidisha nguvu na uwezo wa Iran ya Kiislamu na katika kulinda msingi na asili ya kushirikishwa "Jamhuri" kwa maana ya wananchi katika uchukuaji wa maamuzi muhimu ya taifa.

Siri ya kubakia hai mfumo wa utawala wa Kiislamu hapa nchini ni kuendelea kushikamana kwa mambo mawili yaani Jamhuri (wananchi) na Uislamu, na mahudhurio makubwa ya wananchi katika medani muhimu za kisiasa hususan chaguzi. Ungaji mkono wa wananchi katika mfumo wowote wa kisiasa duniani ni nguvu kubwa ambayo si rahisi kushindwa mbele ya hujuma za aina yoyote ile za maadui na madola ya kibeberu; ni kwa sababu hiyo ndiyo maana utawala wa Kiislamu hapa nchini ungali unapiga hatua za maendeleo licha ya misukosuko na njama nyingi za maadui wake. 

Katika kipindi chote cha zaidi ya miaka 42 iliyopita baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, maadui wametumia mbinu zote zinazowezekana ili kudhoofisha ushirikiano na uungaji mkono wa wananchi kwa utawala wa Kiislamu na hatimaye kuwatenganisha na utawala wao. Lakini kama alivyosema Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, wananchi wameonesha kuwa, daima wanakwenda na kutenda kinyume na matakwa ya adui katika masuala mengi kama katika chaguzi na maandamano yanayofanyika hapa nchini.

Kushirikiana wananchi na utawala wa Kiislamu kunaweza kusaidia sana jitihada za kutatua matatizo mengi na kuzima mashinikizo ya kisiasa na kiuchumi kutoka nje ya nchi. Waziri wa Mambo ya Nje za Nje wa Iran Muhammad Javad Zarif anasema: Wananchi wa Iran ndio wenye taathira kubwa zaidi katika kudhamini uhuru, usalama, hadhi na maendeleo ya nchi. Vilevile kushiriki kwa wingi wananchi katika masuala muhimu ya kitaifa kunalinda maslahi ya kitaifa katika upeo wa kimataifa na kuisaidia nchi katika masuala mbalimbali.

Muhammad Javad Zarif

Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana maadui wanafanya kila wawezalo kuwavunja moyo wa wananchi na kuwahimiza wasitumie haki yao ya kidemokrasia ya kushiriki katika zoezi la uchaguzi wa kesho hapa nchini. Lakini kama alivyosema Ayatullah Ali Khamenei: "Wananchi wameonesha kuwa, daima wanakwenda na kutenda kinyume na matakwa ya adui na kwa taufiki yake Mwenyezi Mungu watashiriki kwa wingi katika zoezi la kupiga kura na kuinua juu hadhi na heshima ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran." 

Tags