Jun 18, 2021 08:02 UTC
  • CNN: Wairani wengi wanashiriki katika zoezi la upigaji kura uchaguzi wa rais

Televisheni ya CNN ya Marekani imeripoti katika kipindi chake maalumu kilichopewa jina la "Uchaguzi wa Iran 2021" kwamba mahudhurio ya Wairani katika zoezi la kupiga kura katika saa za awali mapema leo ni ya kupewa mazingatio.

Wakichambua mipango na mitazamo ya wagombea urais katika uchaguzi wa leo wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, waandishi wa televisheni ya CNN mjini Tehran wameripoti kuwa, idadi kubwa ya watu imejitokeza mapema kupiga kura. 

CNN imeripoti kuwa uchaguzi huu unafanyika huku mazungumzo ya kuhuisha makubaliano ya nyuklia baina ya Iran na nchi za kundi la 4+1 yakiendelea mjini Vienna nchini Austria. Makubaliano hayo yalidumaa baada ya aliyekuwa rais wa Marekani, Donald Trump kuiondoa nchi hiyo kwenye mapatano ya nyuklia ya JCPOA.

Waandishi wa mashirika ya habari ya AFP, Reuters, The New York Times, The Washington Post, Le Monde, Le Fiigaro, Der Spiegel, Zoddeutsche Zeitung, Bild, Austrian Standard, El Pais, France 24, BBC na kadhalika wanachacharika kuripoti matukio ya uchaguzi wa Rais na Mabaraza ya Miji na Vijiji hapa nchini.

Wairani wakipiga kura uchaguzi wa rais

Wizara ya Utamaduni ya Iran imesema kuwa waandishi habari 500 wa kigeni kutoka mashirika 226 ya habari ya kimataifa na mabara matano ya dunia wanaripoti matukio ya uchaguzi wa rais unaofanyika leo hapa nchini Iran.

Wagombea wanne ambao ni Sayyid Ebrahim Raeisi, Mohsen Rezaei, Sayyid Amir-Hossein Ghazizadeh Hashemi na Abdolnaser Hemmati ndio wanaochuana katika uchaguzi wa rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. 

Zaidi ya Wairani milioni 59 elfu 310, (milioni 29, 980,000,38 wanaume na milioni 29,330,000, 269 wanawake) wamekamilisha masharti ya kupiga kura katika uchaguzi wa leo wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.