Jun 18, 2021 12:25 UTC
  • Zarif asisitizia wajibu wa kuondolewa haraka vikwazo vyote vya Marekani

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, kuna wajibu wa kuondolewa haraka vikwazo vyote vya kidhulma vilivyowekwa na Marekani dhidi ya taifa la Iran.

Dk Mohammad Javad Zarif amesema hayo leo wakati alipoonana na Josep Borrell, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya, pambizoni mwa kikao cha Baraza la Diplomasia nchini Italia.

Katika mazungumzo hayo, Zarif amesema wazi kwamba, hakuna mazungumzo mengine yoyote yatakayofanyika wala mapatano mengine ghairi ya haya yaliyopo ya JCPOA. Pamoja na hayo ameelezea matumaini yake ya kufanikiwa mazungumzo ya Vienna yanayohusu namna ya kuimarisha mapatano ya JCPOA.

Pande zilizofikia mapatano ya nyuklia ya JCPOA

 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amegusia vikwazo vichungu vilivyowekwa na Marekani dhidi ya wananchi wa Iran na jinsi Washington isivyo na mwamana na isivyoheshimu ahadi zake na kusema kuwa, ana imani na mazungumzo yanayoendelea hivi sasa huko Vienna kuhusu suala zima la kuondolewa vikwazo vya kidhulma vya Marekani dhidi ya wananchi wa Iran.

Zarif ametoa ufafanuzi pia kuhusu hali ilivyo hivi sasa nchini Afghanistan na kusema kuwa mivutano iliyopo baina ya serikali na mirengo mingine ya kisiasa nchini humo ni moja ya matatizo makubwa ambayo yanauweka kwenye matatizo usalama wa nchi hiyo na nchi jirani.

Kwa upande wake, Josep Borrell, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya ameelezea matumaini yake kuwa mazungumzo yanayoendelea mjini Vienna Austria yatazaa matunda mazuri na makubaliano ya JCPOA yatarejea katika hali yake ya awali.