Jun 21, 2021 02:49 UTC
  • Ujumbe wa Uchaguzi wa Iran katika eneo la Asia Magharibi

Kujitokeza mamilioni ya wananchi wa Iran katika uchaguzi wa 13 wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, siku ya Ijumaa ya tarehe 18 Juni 2021 kumetoa ujumbe wa kila namna katika eneo la Asia Magharibi.

Mosi ni kutokuwa na taathira siasa za vikwazo zilizopigiwa upatu na baadhi ya viongozi wa nchi za Kiarabu kwa kushirikiana na Wazayuni.

Kwa muda mrefu kabla ya kufanyika uchaguzi wa siku ya Ijumaa wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, baadhi ya vyombo vya habari vya nchi za Kiarabu na vya utawala wa Kizayuni wa Israel viliendesha propaganda kubwa kwa lengo la kuwavunja moyo wananchi wa Iran ili kupunguza kujitokeza kwao katika uchaguzi huo kwa shabaha ya kuonesha kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran eti haina uungaji mkono wa wananchi. Maadui hao wenye fikra za Kizayuni waliendesha kampeni kubwa kujaribu kuonesha kuwa vikwazo vya kiwango cha juu vilivyowekwa na rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump vimeathiri vibaya uchumi wa Iran na sasa wananchi wameususia utawala wao na wamekataa kushiriki katika uchaguzi. Lakini njama hizo zimefeli kikamilifu. Katika hotuba yake ya siku ya Jumatano ya tarehe 16 Juni, 2021, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei aligusia njama hizo na kusema kuwa, baadhi ya wale wanaokosoa uchaguzi wa Iran wanashindwa hata kutofautisha baina ya masanduku ya kura na sanduku la matunda.

Watu wamekwenda hata na watoto wao kwenye vituo vya kupigia kura kushiriki kwenye uchaguzi nchini Iran

 

Pili ni umoja na mshikamano wa Wairan katika kukabiliana na njama za adui

Majibu makali na yasiyo na chembe ya kuterereka yaliyotolewa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu dhidi ya maadui hao yalikamilika kwa majibu yaliyotolewa na wananchi wa Iran kwa kujitokeza kwao kwa mamilioni katika masanduku ya kupigia kura. Hivyo ujumbe mwingine wa uchaguzi wa 13 wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ni kwamba wananchi wa Iran si watu wa kuathiriwa na propaganda za maadui na mara zote huwa wanafanya kinyume na anavyowachochea adui. Gazeti la al Banna la Lebanon limeandika: Kwa kweli madola ajinabi yanapaswa kuutambua kikamilifu uhakika kwamba, mara zote Wairani wanakuwa wamoja wenye mshikamano linapokuja suala la kukabiliana na adui kwa ajili ya kulinda uhuru wao. Wakati huo itikadi zao za kisiasa huziweka pembeni.

Tatu ni kupasishwa tena na wananchi wa Iran, mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu

Ujumbe mwengine muhimu unaopatikana katika uchaguzi wa siku ya Ijumaa nchini Iran, ni kwamba kwa mara nyingine, wananchi wa Iran wametangaza uungaji mkono wao kwa mfumo wao wa Jamhuri ya Kiislamu. Wananchi wa Iran wamewaonesha walimwengu kuwa matatizo ya kiuchumi hayawezi kuwazuia kuulinda mfumo wao wa Jamhuri ya Kiislamu na wanatambua vyema kwamba msimamo wao wa kupigania uhuru na ukombozi ndio unaowakasirisha maadui na mabeberu. Zvi Bar'el, mchambuzi wa masuala ya Mashariki ya Kati wa gazeti la Kizayuni la Haaretz ameandika: Kitendo cha kujitokeza wananchi wa Iran katika uchaguzi kina maana ya kutangaza upya uungaji mkono wao kwa utawala ulioko madarakani nchini humo. 

Wananchi wa matabaka mbalimbali wameshiriki kwenye uchaguzi nchini Iran

 

Nne ni kufeli vikwazo vya kiwango cha juu

Moja ya malengo makuu ya siasa za kuwawekea vikwazo vya kiwango cha juu wananchi wa Iran zilizofuatwa na rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump, ni kuwakatisha tamaa wananchi wa Iran na kuwafanya wasijitokeze katika medani za kisiasa kama vile uchaguzi. Hata hivyo kitendo cha karibu nusu ya wananchi wa Iran cha kujitokeza katika uchaguzi wa 13 wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu uliofanyika siku ya Ijumaa, kimefelisha na kusambaratisha njama hizo. Mokhtar Haddad, mchambuzi wa mtandao wa al Ahd wa Lebanon ameandika kuwa, uchaguzi wa Iran umefelisha njama za wale waliokuwa wanajaribu kukwamisha maendeleo ya taifa hilo.

Tano ni kushikamana wananchi wa Iran kukabiliana na jinai za utawala wa Kizayuni huko Palesitna

Wananchi wa matabaka yote walishiriki kwa wingi katika uchaguzi wa siku ya Ijumaa ya tarehe 18 Juni, 2021. Miongoni mwa siasa kuu za Iran ni kuwaunga mkono watu wanaodhululiwa wakiwemo wananchi wa Palestina. Maadui Wazayuni na vibaraka wao wanafanya njama kubwa za kupotosha mapambano hayo. Hata hivyo kujitokeza kwa wingi wananchi wa Iran katika uchaguzi wa Juni 18 kumeonesha kuwa msimamo wao wote ni mmoja katika kadhia ya Palestina. Lakini pia, uchaguzi wa Iran umeonesha mshikamano imara baina ya watu wa matabaka mbalimbali humu nchini katika hali ambayo ni hivi karibuni tu, yaani tarehe 13 Juni, 2021, bunge la utawala wa Kizayuni wa Israel, Knesset, lilikuwa uwanja wa vita baina ya mirengo tofauti, suala ambalo unapolinganisha baina ya mshikamano wa Wairani na ugomvi wa Wazayuni wao kwa wao utaona ni upande gani hasa ulioko kwenye mazingira magumu na dhaifu. Kanali ya televisheni ya al Mayadeen imeripoti kuwa, uchaguzi wa Iran umesikika kwa sauti kubwa huko Tel Aviv na ishara za wahka ndani ya utawala wa Kizayuni zinaonekana waziwazi.

Tags