Jun 21, 2021 05:09 UTC
  • Sayyid Ebrahim Raisi
    Sayyid Ebrahim Raisi

Baada ya uchaguzi wa rais wa Ijumaa iliyopita ambao matokeo yake yamempa ushindi Sayyid Ebrahim Raisi, kunajitokeza swali kwamba, siasa za nje za Iran kuhusiana na eneo la Magharibi mwa Asia zitakuwa vipi katika serikali ijayo ya Tehran?

Serikali mpya ya Jamhuri ya Kiislamu chini ya uongozi wa Sayyid Ebrahim Raisi itaanza kazi zake mwezi Agosti mwaka huu. Katika upande wa kifikra na aidiolojia ya kisiasa, Sayyid Ebrahim Raisi anasanifiwa na kuorodheshwa kuwa ni mtu aliye karibu zaidi na Wahafidhina. Katika masuala ya siasa za nje, mrengo wa Wahafidhina hauna imani na Magharibi hususan Marekani, na unapinga vikali vikwazo dhidi ya Iran japokuwa unaamini suala la kufanya mazungumzo. Hata hivyo mrengo huo unaamini kwamba, si sawa "kuweka mayai yote kwenye kikapu cha mazungumzo" kwa ajili ya kutatua matatizo ya nchi. 

Katika upande wa siasa za kikanda, Wahafidhina wanatoa kipaumbele kwa siasa na sera za muqawama na mapambano na kutanguliza mbele suala la kuwa na uhusiano mwema na mzuri na nchi za Magharibi mwa Asia. Daima wanauona utawala wa Kizayuni wa Israel kuwa ni adui mkubwa wa Iran na Umma wa Kiislamu. Vilevile wanaamini kuwa, kuna ulazima wa kukabiliana na uingiliaji kati wa Marekani katika masuala ya Magharibi mwa Asia. Kwa msingi huo tunaweza kusema kuwa, siasa za serikali ijayo ya Iran kuhusiana na eneo la Magharibi mwa Asia zitajikita zaidi katika mambo matatu:

Kwanza ni kuimarisha mrengo wa muqawama na mapambano dhidi ya utawala haramu wa Israel katika eneo la Magharibi mwa Asia. Kwa sababu hiyo makundi na harakati zote za wanamapambano katika kanda hii zimepongeza sana ushindi wa Sayyid Ebrahim Raisi katika uchaguzi wa rais wa Ijumaa iliyopita nchini Iran. Katika hatua yake ya kwanza mara tuu baada ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi wa rais nchini Iran Wizara ya Mambo ya Nje ya utawala wa Kizayuni wa Israel ilieleza wasiwasi wake mkubwa kuhusiana na kuja madarakani serikali inayounga mkono na kuhami kambi ya mapambano kwa hali na mali nchini Iran. Itakumbukwa pia kwamba, baada ya ushindi wa harakati za mapambano ya ukombozi wa Palestina katika vita vya hivi majuzi vya siku 12, Sayyid Ebrahim Raisi alitoa ujumbe akisema: "Makombora ya wanamapambano yamedhirisha zaidi ulegevu na udhaifu wa usalama kioo wa utawala wa Kizayuni kuliko wakati wowote mwingine; na irada na azma imara ya Wapalestina imeshinda mifumo ya kujikinga na makombo ya Wazayuni."    

Pili ni kwamba, serikali ijayo ya Ebrahim Raisi itafanya jitihada kubwa za kuimarisha uhusiano na nchi zote za Magharibi mwa Asia ikiwemo Saudi Arabia. Sayyid Raisi ana mtazmo wa kidini kuhusiana na siasa za nje. Hata hivyo mtazamo huo wa kidini si wa kimadhehebu au kimakundi, bali anatoa kipaumbele kwa nchi zote za Waislamu za eneo hilo bila ya kujali madhehebu, kaumu na itikadi zao. Rais mteule wa Iran na waungaji mkono wake wanaamini kuwa, inawezekana kudhamini maslahi ya nchi kwa kuimarisha uhusiano na nchi jirani na za kanda hii hususan katika masuala ya uchumi. Wakati alipokuwa akijiandikisha kwa ajili ya kugombea kwenye uchaguzi wa 13 wa Jamhuri ya Kiislamu, Sayyid Ebrahim Raisi alisema kuwa: "Kipaumbele cha siasa za nje za Jamhuri ya Kiislamu ni kushirikiana na nchi zote hususan nchi jirani. Tutashirikiana kirafiki na kwa heshima na wale wasio na uadui na Iran.”

Sayyid Ebrahim Raisi

Kwa msingi huo, kipaumbele cha siasa za nje za serikali ijayo ni kushirikiana na nchi jirani na Jamhuri ya Kiislamu, nchi za Magharibi mwa Asia, Asia ya Kati na Caucasus.

Kipaumbele cha tatu cha siasa za nje za serikali mpya ya Iran ni kukabiliana na ushawishi na uingiliaji kati wa Marekani katika masuala ya kanda ya Magharibi mwa Asia. Sayyid Raisi si mpinzani wa suala la kufanya mazungumzo na Marekani lakini anaamini kuwa, kwa upande mmoja haipaswi kuweka reheni uchumi wa taifa katika mikono ya Marekani; na katika upande mwingine anaamini kuwa, uingiliaji kati wa serikali ya Washington katika masuala ya kanda hii si tu kwamba hausaidii kuimarisha usalama, bali pia ni miongoni mwa sababu kuu zinazovuruga amani na usalama eneo la Magharibi mwa Asia. Sayyid Ebrahim Raisi kama walivyo Wairani wote, anaamini kuwa, Marekani ilifanya jinai kubwa kwa kutekeleza mauaji ya kigaidi dhidi ya Kamanda Qassem Soleimani na kwamba, miongoni mwa majibu yanayopaswa kutolewa kwa jinai hiyo ni kufukuzwa kikamilifu majeshi ya Marekani katika eneo la Magharibi mwa Asia.