Jun 21, 2021 12:43 UTC
  • Sayyid Ebrahim Raeisi
    Sayyid Ebrahim Raeisi

Rais mteule wa Iran amesema kuwa mahudhuria makubwa ya taifa la Iran katika uchaguzi wa rais uliofanyika siku chache zilizopita hapa nchini ni dhihirisho la azma ya wananchi na ujumbe muhimu kwa walimwengu.

Sayyid Ebrahim Raeisi ambaye alikuwa akizungumza na vyombo vya habari kwa mara ya kwanza baada ya kutangazwa mshindi wa uchaguzi wa rais wa Ijumaa iliyopita, amesema kushiriki kwa wingi wananchi wa Iran katika zoezi la kupiga kura licha ya maambukizi ya sasa ya corona, uhasama wa madola ya kibeberu, vita vya kipropaganda na kinafsi ya maadui na matatizo ya kiuchumi yaliyopo, kumetoa ujumbe wa umoja na mshikamano wa Wairani kwa walimwengu. 

Amesema mahudhurio hayo makubwa ya wananchi yametoa ujumbe wa umoja na mshikamano wa kitaifa, udharura wa kufanyika mageuzi katika masuala ya uchumi, kupambana na ufisadi, umaskini na ubaguzi na kwa ujumla kutekeleza uadilifu katika nyanja zote. Sayyid Raeisi amesisitiza kuwa Ijumaa iliyopita Wairan walionesha kwamba, wanashikamana na thamani za Mapinduzi ya Kiislamu na njia ya mashahidi azizi wa mapinduzi hayo hasa Jenerali Shahidi Qassem Soleimani aliyeuawa Januari mwaka jana katika shambulizi la kigaidi la jeshi la Marekani huko Iraq. 

Kuhusu mazungumzo ya nyuklia yanayoendelea huko Vienna kati ya Iran na nchi za Magharibi, rais mteule wa Iran amesema ataunga mkono mazungumzo yanayodhamini maslahi ya taifa lakini hataruhusu mazungumzo kwa ajili ya mazungumzo tu. Amesisitiza udharura wa kuondolewa vikwazo vyote viivyowekwa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu. 

Sayyid Ebrahim Raeisi

Sayyid Raeisi ameihimiza Marekani kutekeleza majukumu yake katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, na kuongeza kuwa watu wa Irani wamesimama imara mbele ya mashinikizo ya Washington yaliyojumuisha vikwazo vikali vya kiuchumi.

Kuhusu msimamo wa Iran juu ya kadhia ya Palestina na mzozo wa Yemen, rais mteule wa Iran amesema: Msimamo wetu ni kwamba watu wa Palestina wanapaswa kupewa haki ya kujiamulia hatima yao kupitia kura ya maoni, na sera ya Jamhuri ya Kiislamu katika kadhia hii itabaki kama ilivyoainishwa na Imam Ruhullah Khomeini. Vilevile ametilia mkazo udharura wa kukomeshwa mashambulio dhidi ya watu wa Yemen wanaoendea kudhulumiwa.

Kuhusu uhusiano wa Jamhuri ya Kiislamu na nchi jirani, rais mteule wa Iran amesema: Tunataka uhusiano mzuri na nchi zote za jirani, haswa Saudi Arabia.