Jun 22, 2021 10:57 UTC
  • Ali Rabei
    Ali Rabei

Msemaji wa Serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa mahudhurio ya wananchi katika zoezi la kupiga kura kwenye uchaguzi wa Rais na Mabaraza ya Miji na Vijiji wa Ijumaa iliyopita yametoa jibu la "hapana" kwa waliotoa wito wa kususiwa zoezi hilo ambao kwa hakika wanashirikiana na maadui walioliwekea vikwazo taifa la Iran.

Ali Rabei amewaambia waandishi wa habari mapema leo mjini Tehran kwamba, wapinzani wa siku zote wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran walianzisha kampeni kubwa dhidi ya uchaguzi huo, mustakbali wa Iran na kuwahamasisha wananchi wasishiriki katika zoezi la kupiga kura, lakini Wairani walitoa jibu la "hapana kubwa" kwa propaganda hizo zote.

Kuhusu msimamo wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani iliyodai kwamba, Wairani hawakuweza kushiriki katika uchaguzi wa rais kwa njia huru na ya haki, Msemaji wa Serikali ya Iran amesema kuwa, matamshi hayo yasiyo na msingi ni kielelezo cha kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine na yanakiuka sheria. 

Ali Rabei

Ali Rabei amesema serikali ya Marekani inapaswa kukoma kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine na kutoa uamuzi kuhusu taratibu za kidimekrasia katika nchi hizo, na badala yake ishughulikie na kurekebisha masuala ya ndani ya nchi hiyo. 

 Kuhusu mazungumzo ya nyuklia yanayoendelea huko Vienna, Msemaji wa Serikali ya Iran amesma: Mazungumzo ya kuhuisha makubaliano ya nyuklia ya JCPOA hayana mfungamano wowote na siasa za ndani wala matokeo ya uchaguzi wa rais bali yanafanyika kwa mujibu wa siasa kuu zilizoainishwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na kwa kutilia maanani maslahi ya taifa.  

Tags