Jun 22, 2021 10:59 UTC
  • Muhammadu Buhari
    Muhammadu Buhari

Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria amemtumia ujumbe rais mteule wa Iran, Hujjatul Islam Walmuslimin Ebrahim Raeisi akimpongeza kwa kuchaguliwa kuwa Rais mpya wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Muhammadu Buhari amesema katika ujumbe huo kwamba, Ayatullah Ebrahim Raeisi alistahiki kushinda uchaguzi wa rais nchini Iran.

Buhari amesema mataifa mawili ya Iran na Nigeria yatafanya jitihada kubwa zaidi za kustawisha ushirikiano na kuongeza kuwa: Uchaguzi wa wananchi wa Iran kwa mara nyingine tena umeonesha umuhimu wa irada na matakwa ya wananchi katika kufanikisha demokrasia kote duniani. 

Rais wa Nigeria amemtaja Ebrahim Raeisi kuwa ni mwanasiasa mwenye tajiriba na uzoefu anayeweza kuiongoza serikali ya Iran hadi kwenye kilele cha juu na mustakbali bora zaidi. 

Uchaguzi wa rais wa Iran ulifanyika Ijumaa iliyopita kote nchini na katika nchi nyingne 133 waliko baadhi ya raia wa Iran. 

Sayyid Ebrahem Raeisi alitangazwa mshindi katika kinyang'anyiro hicho kwa kupata kura milioni 17 na laki 9 na 26,345 za wananchi.

Zaidi ya Wairani milioni 59 walikuwa wametimiza masharti ya kupiga kura katika uchaguzi ambao ulikuwa wa wagombea wanne baada ya Wagombea wengine watatu kujiondoa katika mchuano huo siku ya Jumatano wiki iliyopita.