Jun 23, 2021 03:02 UTC
  • Sayyid Ebrahim Raeisi
    Sayyid Ebrahim Raeisi

Rais mteule wa Iran amesema, katika serikali na utawala wa Kiislamu wafanyakazi wote wanapaswa kujitambua kuwa ni mahadimu na watumishi wa wananchi.

Sayyid Ebrahim Raeisi aliyasema hayo jioni ya jana katika mji mtakatifu wa Mash'had ambako alitoa mkono wa baraka na fanaka kwa Waislamu wote kwa mnasaba wa kuadhimisha siku ya jana tarehe 11 Dhulqaada ya kuzaliwa mjukuu wa Mtume Muhammad (saw), Imam Ali bin Mussa al Ridha (as) na akasema, njia ya kumridhishia Mwenyezi Mungu ni kuwahudumia waja wake. Ameongeza kuwa, maafisa wa serikali wanapaswa kuwapenda wananchi, kwa sababu kuwapenda waja wa Mwenyezi Mungu ndiyo daraja ya chini ya kumpenda Mwenyezi Mungu. 

Sayyid Raeisi amesema wafanyakazi wote wa umma wanapaswa kulinda na kuheshimu utukufu na hadhi ya kila mwananchi. Ameashiria kuwa uadilifu ndio utakaokuwa msingi wa kazi zote za serikali yake na kusema: Kunapaswa kufanyika mageuzi hapa nchini kwa maslahi ya wananchi, thamani za Mapinduzi ya Kiislamu na hali bora ya maisha ya taifa.

Wananchi wa Mash'had wakisubiri hotuba ya Sayyid Ebrahim Raeisi

Rais mteule wa Iran amesema kwamba, yeye kama mwakilishi wa taifa hataruhusu kukanyagwa haki ya mtu yeyote na atafanya jithada kubwa kuhakikisha kwamba, suhula zote za taifa zinagawanywa kwa msingi wa uadilifu.

Vilevile ametilia mkazo udharura wa kudumisha mapambano dhidi ya virusi vya corona na akatoa wito wa kuanza kutolewa chanjo kwa mataba yaliyobakia ya wananchi.