Jun 23, 2021 13:07 UTC
  • Taarifa ya IRIB ya kulaani hatua ya Marekani kuteka tovuti za habari za Iran

Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (IRIB) limetoa taarifa na kulaani hatua ya tovuti zake kadhaa na za mrengo wa muqawama kufungwa na serikali ya Marekani na kusema kitendo hicho ni ukiukwaji wa wazi wa uhuru wa maoni na ni hujuma dhidi ya vyombo huru vya habari.

Taarifa hiyo iliyotolewa Jumatano Wizara ya Sheria ya Marekani imefunga  tovuti za Press TV, Al Alam, Al Kauthar , Al Masira na nyinginezo kwa visingizio visivyo vya kimantki na visivyo na msingi.

Taarifa hiyo imesema hatua hiyo inaashiria sera za kiistikbari na za kibeberu za Marekani na ni ukiukwaji wa wazi na wa makusudi wa sheria za kimataifa.

IRIB imesisitiza kuwa, katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, mitandao ya kijamii ya Facebook, Twitter, Instagram na Youtube, imefunga akaunti za mashirika ya habari na utangazaji ya mrengo wa muqawama kwa visingizo visivyo na msingi jambo ambalo ni kinyume cha sheria za kimataifa katika uga wa uhuru wa maoni.

Taarifa hiyo imesema IRIB itatumia uwezo wake wa kisheria wa kukabiliana na kitendo hicho kiovu cha Marekani. Aidha IRIB imesema tovuti hizo zitakuwa zinatumia domain inayoishia na .ir  badala ya zile zilzofungwa ambazo zilikuwa zinaishia na .com

IRIB imesitiza kuwa itafuatilia kisheria hatua hiyo ya Marekani kukiuka uhuru wa maoni. Kufuatia hatua hiyo Press TV imetangaza kuwa tovuti iliyofungwa ya presstv.com sasa inapatikana kupitia presstv.ir