Jul 23, 2021 10:19 UTC
  • Kiongozi Muadhamu: Viongozi washughulikie utatuzi wa matatizo ya Khuzestan kwa uzito mkubwa

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amevipa jukumu vyombo vya serikali na visivyo vya serikali kuhakikisha vinashughulikia kwa uzito mkubwa utatuzi wa matatizo na masuala ya wananchi wa mkoa wa Khuzestan, kusini magharibi mwa Iran.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ametoa agizo hilo mapema leo mara baada ya kupatiwa dozi ya pili ya chanjo ya corona ya COVIran Barekat iliyotengenezwa hapa nchini.

Akiashiria matatizo ya watu wa Khozestan, Ayatullah Khamenei amesema, katika siku za hivi karibuni moja ya wasiwasi ambao kwa kweli unatia uchungu ni suala la maji Khuzestan na matatizo waliyonayo watu wa Khuzestan.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameeleza alivyosikitishwa na kutotekelezwa maagizo kadhaa aliyotoa huko nyuma kuhusu suala la maji ya Khuzestan na majitaka ya mji wa Ahvaz, makao makuu ya mkoa huo; na akaongeza kwamba, laiti kama maagizo yale yangelitekelezwa bila shaka hali iliyopo sasa isingetokezea ya watu wenye moyo wa uaminifu wa Khuzestan kunung'unika na kuudhika, wakati katika mkoa huo kuna kila aina suhula, vipawa vya kimaumbile pamoja na viwanda.

Ayatullah Khamenei ameeleza kwamba, wananchi wameonyesha jinsi walivyoudhika, lakini haiwezekani kuwalamu kwa sababu suala la maji na katika hali ya hewa ya joto ya Khozestan si jambo dogo.

Bwawa la Karon, ambalo kukauka kwake kumesababisha uhaba mkubwa wa maji Khuzestan

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ameashiria jinsi watu waaminifu na wenye moyo wa kujitolea wa Khozestan walivyokuwa mstari wa mbele wakati wa matatizo ya miaka minane katika Vita vya Kujihami Kutakatifu na akasema: Haipasi watu hawa kusibiwa na matatizo; na laiti kama masuala ya wananchi yangeshughulikiwa kwa wakati, hali hii isingejitokeza.

Lakini sambamba na hayo, Ayatullah Khamenei amewaasa wananchi wajihadhari na njama za adui na akasema, adui anatafuta fursa ya kukitumia kitu chochote kile dhidi ya Mapinduzi, nchi na mambo yenye maslaha na wananchi; kwa hivyo inapasa kuwepo na hadhari ili asipate kutumia kisingizio chochote.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu vilevile ameenzi na kupongeza moyo wa jihadi na juhudi za vyombo vya afya na tiba katika kukabiliana na maradhi, hususan usumbufu mkubwa waliopata wanasayansi na watafiti katika kutengeneza na kuzalisha chanjo ya ndani; na akatilia mkazo ulazima wa kuendelea kuchungwa kikamilifu miongozo ya kiafya mpaka maambukizi ya ugonjwa wa corona yatakaposita.../