Jul 24, 2021 03:53 UTC
  • Uwepo wa kikosi cha wanamaji wa Iran katika maji ya kimataifa; dhihirisho la uwezo wa kulinda usalama baharini

Jukumu la kikosi cha wanamaji cha Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kulinda mipaka ya majini na maslahi ya Iran katika bahari tofauti duniani.

Kikosi cha wanamaji wa Iran kimeimarisha majukumu yake kwa kunyanyua kiwango chake cha ulinzi hadi kufikia kikosi cha kistratijia, jambo ambalo limekifanya kiwe na uwezo mkubwa wa kulinda usalama katika maji ya kimataifa. Akizungumza Jumanne alipokuwa safarini kutembelea Eneo la Kwanza la Kikosi cha Majini cha Iran huko Bandar Abbas, Kamanda wa kikosi cha majini cha Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Admeri Hossein Khanzadi aliashiria maendeleo makubwa ambayo yamepatikana katika kikosi hicho na kusema kwamba ni wazi kuwa maendeleo hayo ambayo yamekifanya kikosi hicho kiweza kudhihirisha uwezo wake mkubwa katika maji ya kimataifa yamefikiwa kutokana na jitihada kubwa ambazo zimefanywa na vijana shupavu wanaopenda na kuyaenzi Mapinduzi ya Kiislamu.

Manowari ya Makran

Kikosi cha Kistratijia cha Wanamaji wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu na pia Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran wameweza kuonyesha uwezo mkubwa katika kulinda usalama wa baharini na hivyo kufikia upeo mkubwa katika kutekeleza majukumu yao katika uwanja huo.

Katika kuendeleza maendeleo hayo, hivi karibuni manowari mpya ya Iran inayojulikana kama Makran ilijiunga na manowari nyingine za Iran katika kulinda usalama wa baharini. Manowari ya Makran imeundwa kwa ajili ya kuwawezesha askari wa majini wa Iran kutekeleza majukumu yao na hasa ya kukabiliana na vitendo vinavyohatarisha usalama katika maeneo ya mbali baharini, na hasa katika maeneo ya Ghuba ya Eden, Bahari ya Sham na Bahari ya Hindi. Manowari hiyo ina zana za kisasa kabisa za kielektroniki, urushaji makombora na za kuwezesha operesheni za ndege zisizokuwa na rubani na maalumu. Manowari hiyo katika kudumisha majukumu ya jeshi la majini la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika bahari za mbali, mwezi Mei uliopita ilitumwa katika Bahari ya Atlantiki.

Meli hiyo sasa imejiunga na manowari nyingine za Iran ikiwemo ya Sahand katika kikosi cha 77 cha Manowari za Iran kwa ajili ya kudhihirisha uwezo mkubwa wa wanamaji wa Iran katika kulinda usalama wa baharini katika Bahari ya Atlantiki. Ni wazi kuwa uwepo huo mkubwa wa baharini unadhihirisha wazi nguvu kubwa ya Iran katika maeneo ya mbali kabisa baharini.

Katika ripoti yake ya karibuni, tovuti ya habari ya Business Insider aliashiria maenedeleo makubwa ambayo yameweza kufikiwa na kikosi cha wanamaji wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kuunda na kukarabati manowari zake na kuongeza kuwa hii leo kikosi hicho kinatuma manowari zake katika bahari tofauti duniani.

Operesheni ya wanamaji ikifanya juu ya manowari ya Makran

Akizungumzia karibuni umuhimu wa suala hilo, Admeri Habibullah Sayyari, Naibu Kamanda Mkuu wa Jeshi la Jamhuriya Kiislamu ya Iran anayesimamia masuala ya uratibu wa jeshi hilo alisisitiza kwamba: Tunaamini kuwa uwepo katika maji ya kimataifa ni haki ya wazi ya jeshi la majini la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na bila shaka tutadumisha njia hiyo kwa nguvu zetu zote.

Kikosi cha majini cha Iran hii leo kina uwezo mkubwa wa kutumia zana na silaha za kisasa kabisa katika kulinda usalama wa fukwe za Ghuba ya Uajemi na Bahari ya Oman hadi katika Bahari za India na Atlantiki na katika nukta nyingine yoyote ya maji ya kimataifa ambayo inahitajia kudhaminiwa usalama wake.

Bila shaka uwepo wa manowari za Iran katika njia nne kuu za kiuchumi baharini, kaskazini mwa Bahari ya Hindi na utekelezaji wa majukumu yake katika Bahari ya Atlantiki ni thibitisho tosha na la wazi la nguvu kubwa iliyonayo Iran katika uwanja huo.