Jul 25, 2021 06:41 UTC
  • Raeisi asisitiza katika mazungumzo na Sultan wa Oman: Maelewano na majirani ni kipaumbele cha serikali mpya ya Iran

Rais mteule wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Ayatullah Seyyid Ibrahim Raeisi amesema kupanua uhusiano na Oman, kwa kuzingatia hali ya kuaminiana kisiasa iliyopo baina ya pande mbili ni lengo lililopo; na kuwa na maelewano na kufanya mazungumzo na mataifa jirani ndicho kipaumbele cha kidiplomasia katika serikali ya 13 ya Iran.

Ayatullah Raeisi ameyasema hayo katika mazungumzo aliyofanya kwa njia ya simu na Sultan Haitham bin Tariq wa Oman.

Mbali na kumpa mkono wa Idi Sultan wa Oman kwa mnasaba wa kusherehekea Sikukuu ya Idul-Adhha, Rais mteule wa Iran amesema, uhusiano wa muda mrefu wa kiudugu wa mataifa mawili ya Iran na Oman na urafiki wa kitambo kati ya nchi mbili ni imara na umekita mizizi, kiasi kwamba haujaweza kudhoofishwa katu na mabadiliko ya kikanda na kimataifa.

Rais mteule wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameuelezea uhusiano wa Iran na Oman kuwa unaoendelea kupanuka na kustawi zaidi na akasema: Pamoja na hayo, maelewano ya Tehran na Muscat bado hayajafikia upeo unaotarajiwa, kwa hivyo inapasa wataalamu wa pande mbili wachukue hatua ya haraka ya kuandaa mpango jumuishi wa kupanua uhusiano wa kiuchumi baina ya nchi mbili utakaotelekezwa baada ya kuidhinishwa na wakuu wa pande mbili.

Rais mteule wa Iran, Ayatullah Seyyid Ibrahim Raeisi

Halikadhalika amesisitiza kuwa, maelewano, mazungumzo, mashauriano na kubadilishana fikra na nchi jirani kuhusu kadhia na masuala muhimu ya eneo, vitakuwa katika kipaumbele cha diplomasia ya serikali ya 13 ya Iran.

Katika mazungumzo hayo ya simu, Sultan Haitham bin Tariq wa Oman, mbali na kumpa mkono wa Idi Ayatullah Raeisi na kumtakia mafanikio katika kipindi chake cha urais, amesema, hana shaka yoyote kuwa uhusiano wa Iran na Oman utaendelea kubaki kuwa imara na kwamba uhusiano huo chanya na wa kirafiki utakuwa na taathira chanya pia kwa matukio yote ya eneo.

Ameongeza kuwa, kuaminiana kisiasa kati ya pande mbili ni miongoni mwa mambo muhimu zaidi yanayozikurubisha pamoja Tehran na Muscat na akasisitiza kwamba nchi yake itaendelea kufuatilia kwa uzito maalum kukurubisha zaidi na zaidi uhusiano wa nchi mbili kwa ajili ya kudhamini maslahi ya eneo zima.../