Jul 27, 2021 02:30 UTC
  • Safari ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar mjini Tehran; anga mpya ya kustawishwa uhusiano baina ya pande mbili

Rais mteule wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Seyyid Ibrahim Raeisi, amesema Iran imethibitisha kuwa ni rafiki na mshirika mwenye muamana na wa kutegemewa na akasisitiza kwamba Jamhuri ya Kiislamu ni yenye kuwatakia mema majirani zake.

Raeisi ameyasema hayo siku ya Jumapili katika mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar Sheikh Muhammad bin Abdulrahman Al Thani aliyekuwa ziarani hapa nchini.

Katika mazungumzo hayo, Rais mteule wa Iran alisema, mataifa mawili ya Iran na Qatar ni ndugu wa kidini na washirika wa kikanda; na akaongeza kuwa: Tehran inaupa umuhimu maalum uhusiano wake na Doha; na nchi jirani zitakuwa na kipaumbele katika sera za nje za serikali ijayo ya Iran.

Rais mteule wa Iran Ibrahim Raeisi (kulia) na Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar Muhammad bin Abdulrahman Al Thani (kushoto)

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar alimpongeza Seyyid Raeisi kwa kuchaguliwa kuwa rais mpya wa Iran na akamfikishia salamu maalum za Amir wa Qatar na akasema: Qatar inataka kuwa na ushirikiano utakaoimarisha uhusiano wa pande mbili  na vilevile kufanya jitihada kwa kushirikiana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ili kuhakikisha amani inatawala katika eneo. 

Mbali na nyuga za kisiasa na kiuchumi, uhusiano wa Iran na Qatar una umuhimu pia kuhusiana na matukio na mabadiliko yanayojiri katika eneo. Moja ya nukta muhimu na ya kuzingatiwa katika uga huo ni sisitizo la rais mteule wa Iran la kujengwa maelewano na kufanywa mazungumzo kuhusiana na masuala ya kikanda na kimataifa.

Nukta nyingine muhimu ni sisitizo la Iran la kudhamini kwa pamoja usalama wa eneo hili na udharura wa kuwepo mashirikiano ya pande mbili na ya pande kadhaa.

Hapo kabla pia, katika mazungumzo aliyofanya hivi karibuni kwa njia ya simu na Mfalme wa Qatar, rais mteule wa Iran alieleza kwamba, Jamhuri ya Kiislamu inataka kuwa na uhusiano mzuri zaidi na majirani zake ikiwemo Qatar. Seyyid Raeisi alisisitiza kuwa, kustawishwa uhusiano wa pande mbili katika kipindi cha mashinikizo na vikwazo kulitoa hakikisho la uendelevu na uthabiti katika uhusiano wa nchi mbili.

Safari ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar mjini Tehran ambayo imefanyika kwa mtazamo huo na sambamba na kukaribia kuingia madarakani serikali mpya ya Iran ina nukta kadhaa muhimu za kuzingatiwa.

Nukta kuu na ya msingi ni kuanzisha utaratibu wa kudhamini "usalama kwa pamoja", ambayo ni mhimili mkuu wa "manifesto ya sera za nje za kikanda" za serikali mpya ya Iran. Kuupa umuhimu msingi huu katika siasa za nje kunaweza kudhamini amani, uthabiti na maendeleo kwa nchi za eneo.

Suala hili limetiliwa mkazo pia katika mazungumzo aliyofanya rais mteule wa Iran na viongozi wa nchi zingine rafiki na jirani. Katika mazungumzo aliyofanya wiki iliyopita na Sultan Haitham bin Tariq wa Oman, Seyyid Ibrahim Raeisi alibainisha kuwa:  maelewano, mazungumzo, mashauriano na kubadilishana fikra na nchi jirani kuhusu kadhia na masuala muhimu ya eneo, vitakuwa katika kipaumbele cha diplomasia ya serikali ya 13 ya Iran.

Kauli hiyo inatilia mkazo ukweli kwamba Iran siku zote iko tayari kufanya mazungumzo na majirani zake. Eneo la Ghuba ya Uajemi hivi sasa linahitaji uhusiano wa kirafiki na kuwepo sauti moja kuliko wakati wowote ule. Kulinda amani na usalama wa eneo hakuhitaji uwepo wa maajinabi wala mashindano ya silaha, bali kunahitaji irada, kujiepusha na uzushaji tuhuma na kuacha kutoa madai hewa na bandia.

Abdullah Saleh Baabud, mtafiti wa masuala ya kimataifa anaielezea hivi taathira chanya ya uhusiano wa aina hiyo kwa mustakbalia wa eneo: "mazungumzo na mashirikiano ya Iran na nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi vinaweza kuliletea eneo amani na uthabiti na kupunguza uwepo wa maajinabi na mashindano ya silaha katika eneo."

Kuwa tayari Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kufanya mazungumzo kwa ajili ya kuleta suluhu na amani, kunatokana na kutilia kwake maanani msingi wa ushirikishaji sauti kadhaa, kufuta kikamilifu uingiliaji wa maajinabi katika mahusiano ya kikanda na kuchukua hatua kwa lengo la kuleta amani endelevu kwa ajili ya wote.

Nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi

Kwa upande wa uhusiano wa kiuchumi pia, kipaumbele cha diplomasia ya kiuchumi ya serikali mpya kitakuwa ni majirani wa Iran. Kwa hiyo kwa kuzingatia mtazamo huo na kiwango cha hali ya kuaminiana iliyopo kati ya Iran na Qatar; tunaweza kusema kwamba, kupanuliwa uhusiano wa Tehran na Doha katika nyuga tofauti za kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni ni lengo linalofikika kikamilifu. Na hasa kutokana na ukweli kwamba, misimamo ya kimantiki iliyoonyeshwa na Iran katika kipindi cha miaka minne ya mzingiro iliokuwa imewekewa Qatar , imezatiti na kuimarisha mafungamano yaliyopo kati ya mataifa haya mawili.../