Jul 29, 2021 02:19 UTC
  • Kusambaratishwa mtandao wa vibaraka wa shirika la ujasusi la Israel: Thibitisho la kuwa macho walinda amani wa usalama wa taifa

Maafisa wa usalama wa Iran wametekeleza vizuri jukumu lao la kufuatilia na kudhibiti habari za kiusalama na intelijensia nje ya mipaka ya nchi, na hatimaye kufanikiwa kusambaratisha mtandao wa vibaraka wanaohudumia shirika la ujasusi la utawala haramu wa Israel, Mosad, ambao walikuwa wamejizatiti kwa zana na silaha nzito kwa nia ya kuingia na kufanya uharibifu nchini.

Huku akifafanua kuwa vibaraka hao walikuwa na nia ya kutumia zana hizo kuchochea machafuko katika miji tofauti, Katibu Mkuu wa Kitengo cha Kukabiliana na Ujasusi cha Wizara ya Intelijensia ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema: Wakati wa kufanyika uchaguzi wa rais nchini hapa pia, utawala wa Kizayuni ulikusudia mara kadhaa kutekeleza operesheni za uharibifu katika pembe kadhaa za nchi ambapo operesheni hizo za kigaidi zilisambaratishwa kufuatia hatua ambazo zilichukuliwa kwa wakati na maafisa usalama wa Iran, na hivyo kutoa pigo kubwa kwa mtandao wa kigaidi wa Mosad katika eneo.

Tangu ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Marekani, utawala haramu wa Israel na washirika wao wa kieneo wamekuwa wakifanya na wanaendelea kufanya njama chungu nzima za kutaka kuuangusha mfumo wa Kiislamu nchini. Katika miaka ya karibuni pia na kufuatia kushindwa siasa za Marekani za mashinikizo ya juu zaidi dhidi ya Iran, pande hizo hasimu zimeamua kuimarisha mashinikizo ya juu kiusalama dhidi ya serikali ya Tehran. Katika uwanja huo kuna ushirikiano wa karibu mno unaofanyika kati ya Marekani, Israel na Uingereza dhidi ya maslahi ya kitaifa ya Iran. Mfano wa wazi katika uwanja huo ni mauaji ya kigaidi ambayo yametekelezwa katika miaka ya karibuni dhidi ya wasomi na wanasayansi wa nyuklia wa Iran.

Shirika la ujasusi la Marekani CIA

Joaf Limour, mtaalamu wa masuala ya kijeshi wa utawala wa Israel anasema kuhusiana na operesheni za kigaidi za utawala huo katika kuwaua kigaidi wanasayansi wa Iran akiwemo Muhsin Fakhrizadeh kwamba: Kile ambacho tumekishuhudia katika miaka ya karibuni ni kubadilika mbinu za Mosad katika muongo mmoja uliopita na baada ya kumuua kigaidi Muhammad al-Mabhuh, mmoja wa viongozi wa Hamas huko Dubai, ambapo shirika hilo limeamua kupunguza hatari ya kuhusisha moja kwa moja maafisa wake katika operesheni za kigaidi na badala yake kutumia vibaraka katika operesheni hizo.

Mtaalamu huyo wa masuala y kijeshi na kiusalama wa utawala wa Kizayuni anaendelea kusema kwamba jambo hilo haliwezi kutekelezeka bila ya msaada wa serikali ya Marekani.

Kwa mujibu wa ripoti kadhaa, shirika la kijasusi la Marekani CIA na lile la utawala ghasibu wa Israel, Mosad, yameimarisha ushirikiano wao kwa ajili ya kuibua ghasia na machafuko ya kikabila katika ardhi ya Iran na hatimaye kuuangusha mfumo wa Kiislamu unaotawala nchini.

Hatua za uharibifu za mashirika hayo ya ujasusi ya Marekani na Israel zimekuwa zikitekelezwa kwa mbinu tofauti ikiwa ni pamoja na kutumia vibaraka wa kijasusi, kuyafadhili kifedha makundi yenye chuki dhidi ya mfumo wa Kiislamu na watu waliohadaika kwa ajili ya kuibua ghasia na machafuko nchini pamoja na kueneza propaganda na vita vya kisaikolojia dhidi ya serikali ya Iran. Katika kukabiliana na njama hizo, vyombo vya usalama vya Iran vimekuwa na mchango mkubwa katika kusambaratisha njama na harakati za maadui na kutoa pigo kubwa dhidi ya mitandao yao ya kijasusi.

Mohsen Fakhrizadeh, mmoja wa wanasayansi wa nyuklia wa Iran aliyeuawa kigaidi na Israel

Kukamatwa kiongozi wa kundi la kigaidi la an-Nidhal ambalo lilihusika na shambulio la kigaidi na ambalo lilisababisha umwagikaji wa damu mwezi Agosti 2018 mjini Ahwaz, shambulio ambalo lilitekelezwa kwa msaada na ushirikiano wa mashirika ya ujasusi ya Saudi Arabia na Utawala wa Kizayuni, kusambaratishwa mtandao wa magendo ya silaha katika mkoa wa al-Borz, kukamatwa timu ya wajasusi watano na vile vile kukamatwa kiongozi wa kundi la kigaidi la Tundar ambalo lilikuwa likiendesha nchini operesheni za kigaidi na uharibifu kwa usimamizi wa Marekani, ni sehemu ndogo tu ya operesheni ambazo zimetekelezwa katika miaka ya karibuni na vyombo vya usalama vya Iran kwa ajili ya kupambana na ugaidi unaodhaminiwa na mataifa ya kigeni.

Kukamatwa vibaraka na majasusi wanaotekeleza ugaidi na vitendo vya uharibifu nchini kwa ushirikiano na usimamizi wa mataifa ya kigeni na hasa ya Magharibi yakishirikiana na washirika wao wa kieneo, kwa hakika ni jambo linalothibitisha wazi uangalifu mkubwa na kuwa macho walinda usalama nchini na vile vile uwezo mkubwa ilionao Iran ya Kiislamu katika kupambana na njama za maadui wa mfumo wa Kiislamu.