Jul 30, 2021 02:21 UTC
  • Iran yaahidi kuendelea kulitetea taifa linalodhulumiwa la Palestina

Naibu mjumbe wa Irani katika Umoja wa Mataifa amekemea kimya cha miongo saba cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mbele ya vitendo vyote visivyo halali vinavyofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israeli, akisema historia ya wanadamu inashuhudia kwamba, wakati vitendo visivyo halali na uhalifu unapoachwa bila ya kuchukuliwa hatua hukaririwa na kufanywa tena.

Zahra Ershadi ambaye alikuwa akizungumza kabla ya kikao cha Baraza la Usalama la UN kuhusu "Hali ya Mashariki ya Kati, ikiwemo Palestina amesema kimya cha muda mrefu cha Baraza la Usalama na kutochukua hatua vimeuhamasisha utawala huo kutenda jinai na uhalifu mkubwa zaidi. 

Vilevile ameikosoa Marekani kwa kuihamasisha zaidi Israeli kutokana na kuikingia kifua na kuulinda utawala huo ghasibu mbele ya hatua yoyote na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Amesema mfano wa hivi karibuni wa ukweli huo ni kitendo cha Marekani mwezi Mei mwaka huu wa 2021, cha kulizuia Baraza la Usalama kutoa hata taarifa nyepesi kwa waandishi wa habari inayotaka kukomeshwa mashambulizi ya Israeli dhidi ya raia wa Ukanda wa Gaza.

Ershadi ameweka wazi kuwa "msaada na kinga hiyo ya Marekani kwa Israeli inapingana na haki za Wapalestina wanaodhulumiwa, ikiwemo haki yao ya kuishi, kuwa na heshima, kuwa huru, kujilinda, kujitawala, na kuanzisha dola lao huru.

Watoto wa Palestina waliouawa katika mashambulizi ya Israel

 

Mwanadiplomasia huyo wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa: “Baraza la Usalama linapaswa kukomesha mara moja mwenendo huu ambao haukubaliki na hauwezi kuhalalishwa na kuulazimisha utawala wa Israeli kukomesha mara moja uhalifu wake wote dhidi ya Wapalestina; kuondoa mzingiro usio halali na wa kinyama dhidi ya Ukanda wa Gaza; kuondoka katika ardhi zote zilizoghusubiwa ya Palestina, Golan huko Syria na sehemu ya ardhi ya Lebanon. Vilevile Zahra Ershadi ametoa wito wa kuwajibishwa utawala wa Kizayuni wa Israel kwa kutenda uhalifu mkubwa wa kimataifa kwa miongo kadhaa. 

Amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inalaani utawala wa Israeli kwa maneno makali na inasisitiza uungaji mkono wake kwa mapambano ya haki ya watu wa Palestina na kutambua kikamilifu haki zao zote ambazo haziwezi kutenganishwa, haswa haki yao ya kujitawala na kuanzisha nchi huru ya Palestina, mji mkuu wake ukiwa Quds.