Jul 30, 2021 02:21 UTC
  • Matamshi ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu katika kikao cha mwisho na serikali ya duru ya 12

Akizungumza Jumatano asubuhi katika kikao cha mwisho na Rais Hassan Rouhani pamoja na serikali yake ya duru ya 12, Ayatullah Ali Khamenei ametoa hotuba muhimu ambapo ameashiria malengo ya Marekani kudumisha uadui wake dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu na kubainisha nukta kadhaa katika uwanja huo.

Amesema: Imebainika wazi katika serikali hii kwamba kuwategemea Wamagharibi hakuna faida yoyote na wala hawasaidii chochote. Huwa wanatumia kila fursa inayojitokeza kutoa pigo na wasipotoa pigo huwa tu wameshindwa kufanya hivyo.

Kiongozi Muadhamu pia ameashiria mazungumzo ya karibuni huko Vienna Austria na kusema: "Wamarekani hutoa ahadi tupu kuwa tutaondoa vikwazo lakini hawajaviondoa na wala hawataviondoa. Isitoshe, wanatoa sharti na kusema ni lazima muongeze kwenye mazungumzo haya sentensi inayosema kwamba baadaye tutajadili baadhi ya mambo, la sivyo hatutafikia mapatano."

Ayatullah Khamenei amesema, kwa kuongeza sentensi hiyo wanataka kujipa kisingizio cha baadaye kuingilia na kuvuruga nguzo muhimu za mapatano ya nyukilia ya JCPOA, makombora ya Iran na masuala mengine ya kieneo.

Iran kutoiamini Marekani si nara tu bali ni matokeo ya uzoefu mkongwe, tabia na mienendo ya hivi sasa ya Marekani na uchambuzi unaozingatia ukweli wa mambo na malengo halisi ya kibeberu ya nchi hiyo ya Magharibi. Kushindwa kufikiwa malengo yaliyoainishwa wazi katika mapatano ya JCPOA kunatokana na ukweli mchungu wa baadhi ya mambo ambayo yamechochewa na pande zinazofahamika vizuri. Mienendo ya Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya zikiwemo Ufaransa na Uingereza imeenda nje ya mipaka ya mapatano hayo ya kimataifa na sasa inagusa masuala nyeti ya ulinzi wa taifa la Iran. Mienendo hiyo bila shaka inalenga kuingilia mambo ya ndani na hatimaye kuidhoofisha Iran.

Rais Rouhani na baraza lake la mawaziri katika kikao cha Jumatano

Miaka mitano iliyopita, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alizungumzia kwa undani suala hilo na kusema: "Hii JCPOA kwetu sisi imekuwa ni mfano na uzoefu..... Kidhahiri wao hutoa ahadi nzuri na za kuvutia kwa kutumia lugha laini na tamu lakini kivitendo huwa wanafanya njama, uharibifu na kutekeleza vitendo vya kuzuia maendeleo yetu."

Swali linalojitokeza hapa ni kuwa je, Marekani inafuatilia malengo gani kwenye mazungumzo na ni kwa nini inasisitiza kwamba ni lazima yaendelee?

Ni wazi kuwa lengo la mwisho la Marekani ni kutaka kuudhibiti mfumo wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Murad Enadi, mtaalamu wa masuala ya kisasa anachambua baadhi ya malengo yanayofuatiliwa na Marekani kupitia mazungumzo hayo na kusema: ".....Marekani inadumisha vikwazo vilivyopasishwa na Congress dhidi ya Iran tarehe 2 Agosti 2017 na wakati huo huo kutekeleza siasa mpya za vikwazo katika fremu ya CAATSA. Kwa kutumia visingizio tofauti kama haki za binadamu au kuwa eti Iran inaunga mkono ugaidi, kivitendo imeanzisha vikwazo vingine vipya na kuviimarisha zaidi kwa kutumia mbinu mpya."

Uzoefu unaonyesha kuwa Iran imeishinda Marekani mara kadhaa katika mazungumzo ambayo yamefanyika katika nyakati tofauti.

Kwa kutilia maanani jambo hilo, ni wazi kuwa maneno ya Kiongozi Muadhamu yanapasa kupewa uzito na kuchukuliwa kuwa ni kiashiria na kipimo kwa ajili ya serikali ijayo ya 13 kuhusiana na suala zima la mapatano ya JCPOA. Hii ni kutokana na ukweli kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haina nia ya kupoteza wakati na nguvu zake kwa kutegemea ahadi tupu na zisizo na maana, zinazotolewa mara kwa mara na nchi za Magharibi kuhusu kadhia hiyo. Jambo lenye umuhimu kwa kizazi cha leo na cha kesho cha Iran ni kutumiwa vizuri uwezo wa ndani ya nchi na hasa katika sekta ya uchuimi.

Baadhi ya waliohudhuria kikao hicho

Jambo lisilo na shaka ni kuwa serikali ya Marekani inatumia mbinu, njama na nguvu zake zote kuipigisha magoti Iran lakini ni wazi kuwa haitafanikiwa kufikia lengo lake hilo kutokana na uzoefu mkubwa ilionao Iran kuhusu tabia na siasa za Marekani kuhusu mapatano ya JCPOA.

Katika ripoti yake ya karibuni kwa Congress ya Marekani, Antony Blinken, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani alisema anataraji kuwa vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran vitaendelea kutekelezwa hata kama pande mbili zitafikia mapatano na kurejea katika utekelezaji wa JCPOA.

Kwa kutilia maanani uvunjaji ahadi wa Marekani, ni wazi kuwa Iran ina shaka na wasi wasi mkubwa kuhusu ahadi zinazotolewa na nchi hiyo. Kama alivyoashiria Kiongozi Muadhamu, hivi sasa pia Marekani bado haina haya wala aibu ya kuendelea kuvunja ahadi zake kwa mataifa mengine na hasa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, na hili bila shaka ni somo na funzo muhimu kwa serikali na wanasiasa wa baadaye na pia wanaharakati wote wa kisiasa nchini.