Jul 30, 2021 08:05 UTC
  • Zarif amwandikia barua Katibu Mkuu wa UN kuelezea jinsi Marekani na Wamagharibi walivyohalifu ahadi

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amemwandikia barua Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kubainisha jinsi Marekani na Wamagharibi walivyohalifu ahadi na utekelezaji wa majukumu yao katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.

Katika barua hiyo aliyomwandikia Antonio Guterres kwa mnasaba wa kutimia mwaka wa sita tangu lilipopitishwa azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Mohammad Javad Zarif amebainisha vipengee mbalimbali vya jinsi pande za Magharibi zilivyohalifu ahadi na kukwepa kutekeleza majukumu yao; na akayasajilisha hayo kuwa hati na nyaraka rasmi katika Sekretarieti ya Umoja wa Mataifa.

Barua hiyo ya Zarif iliyoambatanishwa na nyaraka za muda wa miaka sita za ushahidi wa jinsi Magharibi ilivyohalifu kutekeleza makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, ambazo waziri huyo wa mambo ya nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alizialifu katika minasaba mingine tofauti huko nyuma imechapishwa ikitanguliwa na utangulizi aliouandika yeye mwenyewe kwa lugha mbili za Kifarsi na Kiingereza.

Majimui nzima ya hati na nyaraka hizo pamoja na maelezo yake, ambayo yameandaliwa na waziri Zarif imekusanywa na kituo cha mitaala ya kisiasa na kimataifa cha wizara ya mambo ya nje ya Iran katika kabrasha la kurasa 200 ambalo nakala yake ya kidigitali inaweza kupatikana hivi sasa na watu wote.

Kwa mujibu wa kituo hicho, nakala za kitabu za majimui ya nyaraka hizo zitaweza kupatikana madukani kuanzia wiki ijayo.

Kwa mujibu wa azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa vikwazo vyote vya silaha ilivyokuwa imewekewa Iran vilifutwa.

Hata hivyo hadi sasa na kinyume na maazimio ya Umoja wa Mataifa, serikali ya Marekani haijatekeleza ahadi na jukumu lake lolote kuhusiana na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.../