Jul 31, 2021 11:44 UTC
  • Barua ya Iran kwa Katibu Mkuu wa UN: Serikali ya Marekani haijatekeleza majukumu yake ndani ya mapatano ya JCPOA

Serikali ya Marekani hadi sasa haijatekeleza majukumu yake ndani ya mapatano ya nyuklia ya JCPOA kinyume na maazimio ya Umoja wa Mataifa.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Muhammad Javad Zarif katika barua yake aliyomtumia Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa mnasaba wa kutimia mwaka wa sita tangu kupasishwa azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la umoja ambapo ameorodhesha ukengeukaji wa nchi za Magharibi wa makubaliano hayo na kuusajili kama ushahidi na waraka rasmi katika sekretarieti ya Umoja wa Mataifa. 

Makubaliano ya nyuklia ya (JCPOA) yalisainiwa Julai 14 mwaka 2015 baada ya miaka 13 ya mazungumzo ya vuta nikuvute. Baada ya wiki moja, mapatano hayo yalipasishwa kupitia azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Mapatano hayo yameainisha wazi majukumu yanayopaswsa kutekelezwa na kila upande katika fremu ya azimio hilo la Baraza la Usalama majukumu; hata hivyo Rais wa Marekani aliyeshindwa katika uchaguzi wa rais uliopita, Donald Trump, tarehe 8 Mei mwaka 2018 alitangaza rasmi kuiondoa nchi hiyo katika mapatano hayo ya kimataifa. Utawala wa Rais Joe Biden pia bado haujatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa mapatano ya JCPOA. 

Mapatano ya JCPOA yaliyopasishwa na Baraza la Usalama la UN 

Akizungumza Jumatano iliyopita katika kikao chake mwisho na Rais na viongozi wa Serikali ya Awamu ya 12, Ayatullah Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alisema: "Wamarekani hutoa ahadi tupu kuwa wataondoa vikwazo dhidi ya Iran lakini hawajaviondoa na wala hawataviondoa. Isitoshe, wanatoa sharti kwamba, lazima muongeze kwenye mazungumzo hayo kipenge kinachosema kwamba, baadaye tutajadili baadhi ya mambo, la sivyo hatutafikia mapatano." Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu aliongeza kusema kuwa: Kwa kuongeza sentensi hiyo wanataka kujipa kisingizio cha baadaye kuingilia mapatano ya nyukilia ya JCPOA, makombora ya Iran na masuala mengine ya kieneo. 

Ayatullah Khamenei katika mazungumzo na Serikali ya Awamu ya 12 inayomaliza muda wake 

Katika miongo ya karibuni Marekani imedhihirisha kuwa si nchi inayoweza kuheshimu makubaliano yoyote ya kimataifa. Mapatano ya JCPOA pia hayakusalimika ya mienendo hiyo miovu ya Marekani. 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres hivi karibuni na katika ripoti yake ya 16 alieleza kwamba anatiwa wasiwasi na mchakato wa utekelezaji wa azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama na kuitaka Washington kuindolea Iran vikwazo.

Naye Mikhail Ulyanov mwakilishi wa Russia katika taasisi za kimataifa huko Vienna Ijumaa ya jana alikumbusha katika ukurasa wake wa Twitter kwamba: "Lengo kuu pekee la mazungumzo ya Vienna ni kuhuisha mapatano ya JCPOA." 

Ukiukaji wa mapatano ya JCPOA yenye umri wa miaka 6 tangu kupasishwa azimio nambari 2231 umefikia kiwango cha tahadhari. Kwa sasa Marekani haijakidhi matakwa ya Iran kwa mujibu wa vipengee vya JCPOA ya kuondoa vikwazo vyote vilivyowekwa wakati wa utawala wa Rais Trump. Ni dhahir shahir kuwa, Wamarekani hawako tayari kuondoa kikamilifu vikwazo dhidi ya Iran na kutoa hakikisho kwamba haitakariri hatua na misimamo yake sawa na ile ya serikali iliyotangulia kuhusu mapatano ya JCPOA. Vilevile Marekani haiko tayari kukubali ukweli kwamba, matatizo ya sasa yamesababishwa na hatua na misimamo yake isiyo ya kimantiki na matakwa yake ya kujitanua na upande mmoja.  

Kazem Gharibabadi Balozi na mwakilishi wa kudumu wa Iran katika taasisi za kimataifa huko Vienna, Austria amesema: Marekani na nchi za Magharibi kwa ujumla zilikuwa zikitaka kutimiza malengo yao katika mazungumzo hayo na jambo hilo linaonesha jinsi nchi hizo zinavyoyatizama mapatano hayo ya nyuklia kama ngazi ya kupitia na kuingilia masuala mengine yasiyo na mfungamano na kadhia hiyo kama masuala ya kieneo na makombora ya Iran."

Kazem Gharibabadi, Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika taasisi za kimataifa zenye makao mjini Vienna Austria

Barua ya Iran kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika kumbukumbu ya kutimia mwaka wa sita tangu kupasishwa azimio nambari 2231 kwa hakika inakumbusha irada na azma ya Tehran ya kuyalinda mapatano ya JCPOA. JCPOA ni mapatano yaliyofikiwa na pande kadhaa, kwa msingi huo, haitarajiwi kuwa yatakuwa na matunda ya kuridhisha iwapo yatatekelezwa na upande mmoja.