Jul 31, 2021 13:42 UTC
  • Balozi Barmaki: Iran na Kenya ziko katika mkondo wa kustawisha uhusiano wa kiuchumi

Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Nairobi Kenya amesema kuwa, Kenya ni nchi muhimu sana kwa Iran na kusisitiza kwamba, siku zote kumekuwa kukifanyika juhudi za kuhakikisha uhusiano wa pande mbili unakua na kuchukua wigo mpana zaidi.

Dakta Jafar Barmaki amesema hayo katika mahojiano maalumu na Shirika la Habari la Iran Press na kusema kuwa, Kenya ikiwa moja ya nchi muhimu katika eneo la Afrika Mashariki inahesabiwa kuwa Lango la kuingia barani Afrika na kwamba, kuwa na uhusiano na nchi hii ni jambo lenye umuhimu katika sera za kigeni za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Kenya ameongeza kuwa, mwaka huu ni mwaka wa 50 wa uhusiano wa kidiplomasia na Kenya na kwamba, ubalozi wa Iran mjini Nairobi utafanya sherehe maalumu kwa ajili ya kumbukumbu hii.

Bendera  za Kenya na Iran

 

Balozi Barmaki kadhalika amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina uhusiano na ushirikkiano na Kenya katikia nyanja mbalimbali ambapo katika uga wa uchumi kwa mara ya kwanza kumeanzishwa Kituo cha Ubunifu na Teknolojia cha Iran (IHIT) katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi. na hivyo kuandaa uwanja wa kuweko bidhaa za Iran katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Aidha amesema, katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, Kenya imekuwa mshirika wa pili wa kibiashara wa Iran barani Afrika na kwamba, kuna matumaini huko mbeleni uhusiano wa Tehran  na Nairibi utakuwa na kuimarika zaidi na zaidi.

Tags