Aug 03, 2021 06:35 UTC
  • Sheikh Issa Qassim atuma ujumbe wa pongezi kwa kuachiliwa huru Sheikh Ibrahim Zakzaky

Kiongozi wa Kiroho wa Harakati ya Wananchi wa Bahrain ametuma ujumbe wa pongezi kwa Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria kwa kuachiliwa kwake huru.

Ayatullah Issa Qassim amesema katika ujumbe wake huo wa pongezi kwa Sheikh Zakzaky: Siku ya kuachiliwa kwako huru kutoka katika gereza la madhalimu, ni siku ya furaha ya kweli kwa waumini na watu wote wanaotambua thamani ya mtu mfano wako katika kuunga mkono na kutetea uhuru na udugu na kufanya juhudi za kueneza haki za uadilifu.

Sheikh Issa Qassim amesisitiza akimhutubu Sheikh Zakzaky kwamba: Kwa hakika jihadi, subira na kusimama kwako kidete kumewafedhehesha madhalimu.

Katika sehemu nyingine ya ujumbe wake wa pongezi Sheikh Issa Qassim amemuomba Mwenyezi Mungu ampatie afya njema na uzima kamili Sheikh Ibrahhim Zakzaky pamoja na mkewe mpendwa, na awape nguvu ya kuendelea kusimama kidete.

Sheikh Ibrahim Zakzaky na mkewe Malama Zeenat

 

Sheikh Ibrahim Zakzaky na mkewe Malama Zeenat waliachiwa huru Jumatano iliyopita baada ya kushikiliwa mahabusu kwa kipindi cha miaka 6 na kukabiliwa na mateso na sulubu nyingi. 

Kwa mujibu wa duru za habari, baada ya vyombo vya dola kumshikilia kiongozi huyo wa kidini kwa muda wote huo, hatimaye mahakama ya nchi hiyo imemtoa hatiani Sheikh Zakzaky na mkewe kuhusiana na mashtaka yote yaliyokuwa yakiwakabili.

Sheikh Ibrahim Zakzaky na mke wake walikamatwa Desemba 13, 2015 katika hujuma na shambulio lililofanywa na askari wa jeshi la serikali dhidi ya Husainiya iliyoko katika mji wa Zaria.

Tags