Aug 04, 2021 00:57 UTC
  • CNN: Raeisi hatalegeza kamba hata kiduchu mbele ya Marekani

Televisheni ya CNN ya Marekani imeripoti kwamba, kwa rais huyu mpya wa Iran, Tehran haitarudi nyuma hata kidogo mbele ya Marekani, na kuchaguliwa kwa Ebrahim Raeisi kuwa Rais wa Iran kutakuwa na matunda makubwa kwa Jamhuri ya Kiislamu.

Televisheni ya CNN ambayo ilirusha moja kwa moja sherehe ya kuidhinishwa rasmi Ebrahim Raeisi kuwa Rais wa Serikali ya 13 ya Jamhuri ya Kiislamu, imetangaza kuwa, Raeisi amesema  Iran itakuwa na siasa za nje amilifu na imara na kwamba haitalegeza kamba hata kidogo mbele ya Marekani.

Kanali hiyo ya televisheni ya Marekani imeongeza kuwa, suala hili linapaswa kupewa mazingatio, kwa sababu Raeisi ameyasema hayo katika matamshi yake ya kwanza baada tu ya kuidhishwa kuwa rais mpya wa Iran. Imesema: Alipoulizwa kwamba, je atakutana na kufanya mazungumzo na Rais Joe Biden wa Marekani, Rais mpya wa Iran amejibu kwa kusema, "hapana, hili halitafanyika". 

Sayyid Ebrahim Raeisi

Televisheni ya CNN imeongeza kuwa: "Hapana shaka kuwa Wairani watakuwa na misimamo mikali zaidi kuhusu makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kwamba pande mbili bado zina hitilafu nyingi katika baadhi ya mambo na zinafanya jitihada za kufikia mapatano. Hata hivyo katika masuala yanayohusiana na mivutano ya eneo la Magharibi mwa Asia, hususan baina ya Iran na Marekani, Rais mpya wa Iran hatalegeza kamba au kurudi nyuma hata kiduchu."

Serikali mpya ya Marekani chini ya ungozi wa Joe Biden sambamba na kukiri kwamba mashinikizo ya kiwango cha juu ya Washington dhidi ya Tehran yamefeli lakini hadi sasa haijachukua hatua ya maana ya kurekebisha siasa hizo za utumiaji mabavu.