Aug 04, 2021 03:02 UTC
  • Iran yakanusha uvumi kwamba vikosi vyake vya ulinzi vimeingia ndani ya meli zinazopita katika Ghuba ya Uajemi

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekanusha vikali madai ya baadhi ya vyombo vya habari vya Magharibi na vya Kizayuni vilivyodai kwamba vikosi vya ulinzi vya Iran vimeingia ndani ya meli zinazopita katika Ghuba ya Uajemi na Bahari ya Oman.

Saeed Khatibzadeh amesisitiza kuwa uvumi ulioenezwa kwamba vikosi vya ulinzi vya Iran vimeingia ndani ya meli zinazopita katika eneo la Ghuba ya Uajemi na Bahari ya Oman hauna ukweli wowote na akatahadharisha kuhusu uenezaji habari za uongo unaofanywa na vyombo vya habari vya Magharibi na vya Kizayuni.

Aidha kutokana kuenezwa habari zenye migongano kuhusu usalama wa vyombo vya majini katika eneo, Khatibzadeh amezitaka pande zote kuwa macho kuhusiana na uenezwaji wa habari bandia na za kubuni.

Mapema kabla ya kutoa tamko hilo, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alitangaza kuwa, kuenezwa habari za kujiri mlolongo wa matukio yaliyolenga meli zinazopita katika eneo la Ghuba ya Uajemi na Bahari ya Oman ni jambo lenye kutia shaka kubwa na akatoa tahadhari juu ya uenezaji habari za uongo kwa malengo machafu ya kisiasa.

Saeed Khatibzadeh

Pamoja na hayo, Khatibzadeh amesisitiza tena kuhusu sera za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran za kulinda na kudumisha amani na uthabiti katika eneo la Ghuba ya Uajemi na Bahari ya Oman na akasema, endapo utahitajika msaada, vikosi vya wanamaji vya Iran viko tayari kutoa huduma za usaidizi kwa meli zinazopita katika eneo hilo.

Usiku wa kuamkia leo, baadhi ya vyombo vya habari viliripoti kuwa yametokea matukio kadhaa yaliyolenga meli zinazopita kwenye pwani ya Imarati.

Kuhusiana na habari hiyo, shirika la habari la Associated Press lilidai kwamba, uongozaji meli zisizopungua nne katika pwani ya Imarati umetoka nje ya udhibiti wa manahodha wa meli hizo.

Baada ya ripoti hiyo vyombo vya habari vya uenezaji uvumi vya Kiingereza na Kizayuni, likiwemo shirika la habari la Reuters vilidai kuwa, vikosi vya ulinzi vya Iran vimedhibiti meli kadhaa katika eneo hilo.../