Aug 04, 2021 08:02 UTC
  • Viongozi waalikwa waendelea kuwasili nchini kuhudhuria hafla ya kuapishwa rais mpya wa Iran

Waziri wa Mambo ya Nje wa Bosnia Herzegovina na waziri wa utalii wa Ghana wamewasili mjini Tehran kuhudhuria hafla ya kuapishwa rais mpya wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Bisera Turković , Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri, na Waziri wa Mambo ya Nje wa Bosnia Herzegovina na Ibrahim Muhammad, Waziri wa Utalii wa Ghana waliwasili mjini Tehran mapema jana kuhudhuria hafla ya kuapishwa Sayyid Ibrahim Raeisi, kuwa rais mpya wa Iran.

Hamuda Sabagh, Spika wa Bunge la Syria ambaye naye pia amekuja nchini kwa madhumuni ya kuhudhuria hafla ya kuapishwa rais mpya wa Iran alipowasili mjini Tehran alilakiwa na Abbas Golru, mjumbe wa kamati ya usalama wa taifa na sera za nje ya Bunge,ambaye pia ni naibu mkuu wa kundi la urafiki la mabunge ya nchi mbili.

Viongozi wengine ambao wameshawasili mjini Tehran hadi sasa ni pamoja na Spika wa Bunge la Tanzania Job Ndugai, Spika wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar Zubeir Ali Maulid pamoja na maspika wa mabunge ya Tajikistan Uzbekistan na Niger.

Hafla ya kuapishwa rais mpya wa Iran itafanyika kwenye ukumbi wa Bunge

Hadi sasa, tayari viongozi na maafisa 115 kutoka nchi 73 duniani wamethibitisha kuwa watahudhuria hafla ya kuapishwa Sayyid Ibrahim Raeisi. Miongoni mwao ni viongozi 10, wakiwemo marais na wakuu wa nchi, maspika wa bunge 20 mawaziri 11 wa mambo ya nje, mawaziri wengine 10 na vilevile wawakilishi maalum, manaibu spika wa mabunge pamoja na wakuu wa kamati za mabunge.

Wakuu na wawakilishi wa mashirika mbalimbali ya kikanda ana kimataifa, mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Katibu Mkuu wa OPEC, na maafisa kutoka IPU, Umoja wa Ulaya, Eurasia, Umoja wa Mabunge ya Nchi za Kiislamu na za Asia, Jumuiya ya ECO na kundi la D8 nao pia watahudhuria hafla hiyo.

Sayyid Ibrahim Raeisi, ataapishwa kuwa rais mpya wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kesho Alkhamisi katika ukumbi wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, yaani Bunge la Iran.../