Aug 05, 2021 07:57 UTC
  • Raeisi: Uhusiano wa Tehran na Muscat umetokana na maingiliano na masuala ya kihistoria ya mataifa mawili

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa uhusiano wa Tehran na Muscat ni zaidi ya uhusiano wa nchi mbili jirani na umetokana na maingiliano na masuala ya historia baina ya nchi mbili.

Rais wa Iran amebainisha hayo katika mazungumzo hapa Tehran na Badr bin Hamad al Busaidi Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman ambaye pia ni Mjumbe Maalumu wa Sultan wa Oman.

Rais Sayyid Ibrahim Raeisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akiashiria kuwa, uhusiano mwema wa Iran na Oman haujasalia tu katika kiwango cha uhusiano wa pande mbili bali nchi mbili hizi zimekuwa na uhusiano katika ushirikiano na maelewano kati ya nchi mbili katika uga wa kimataifa na kieneo pia ameongeza kuwa: Lengo la Jamhuri yaKiislamu ni kustawisha uhusiano na Oman katika nyanja zote za kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni.

Rais wa Iran, Ibrahim Raeisi

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria namna nchi za eneo zilivyo na nguvu na uwezo wa kudhamini usalama wa eneo la Mashariki ya Kati na kueleza kuwa uwepo wa nchi ajinabi katika eneo hauna taathira yoyote ya maana ghairi ya kutishia usalama. 

Katika mazungumzo hayo, Badr bin hamad al Busaidi Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman ameeleza kuwa, amebeba ujumbe wa pongezi na salamu za dhati kutoka kwa Sultan wa Oman kwa ajili ya Rais Mpya wa Iran. Amesema uhusiano kati ya Iran na Oman umekuwa kigezo cha uhusiano kati ya nchi za eneo na kwamba nchi mbili zinajivunia uhusiano huo wa kihistoria na wa siku nyingi.