Aug 12, 2021 08:11 UTC
  • Iran yatoa mkono wa pole kwa taifa la Algeria kufuatia makumi kuuawa na moto misituni

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameeleza masikitiko yake baada ya moto mkubwa unaoendelea kuteketeza misitu nchini Algeria, kuua makumi ya watu na kuwaacha wengine wengi bila makazi.

Saeed Khatibzadeh leo Alkhamisi ameeleza masikitiko yake kufuatia moto mkubwa ulioathiri misitu ya maeneo ya kaskazini mwa Algeria na kusababisha maafa makubwa ikiwa ni pamoja na kusababisha vifo vya makumi ya watu.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu iko pamoja na serikali na taifa rafiki na ndugu la Algeria na ametoa mkono wa pole kwa familia za watu waliopoteza maisha katika ajali hiyo ya moto.

Hii ni katika hali ambayo, idadi ya watu waliopoteza maisha baada ya moto mkubwa kuteketeza misitu katika mkoa wa kaskazini mwa nchi wa Tizi Ouzou imepindukia 60.

Moto mkubwa unaoteketeza misitu ya Algeria

Msemaji wa Idara ya Huduma za Dharura ya nchi hiyo, Nassim Barnaoui  amesema moto huo ulioanza siku ya Jumatatu hadi sasa umesababisha vifo vya watu 69. 

Habari zaidi zinasema kuwa, zaidi ya visa 70 vya misitu kuteketea kwa moto vimeripotiwa katika mikoa 18 ya kaskazini mwa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika katika siku za hivi karibuni.

Wakati baadhi ya viongozi wa Algeria wakisema kuwa, chanzo cha moto huo ni kupanda kwa kiwango cha joto, ushahidi unaonyesha kuwa, chanzo cha moto huo ni sababu za kibinadamu.

Tags