Aug 24, 2021 07:40 UTC
  • Iran yataka kupelekwa misaada zaidi ya kibinadamu nchini Syria

Msaidizi Mwandamizi wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika Masuala Maalumu ya Kisiasa ametoa mwito wa kupelekwa nchini Syria misaada zaidi ya kibinadamu.

Ali-Asghar Khaji ametoa mwito huo katika mazungumzo yake ya simu na Geir O. Pedersen, Mjumbe Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Masuala ya Syria ambapo wamejadili hali na matukio ya hivi sasa katika nchi hiyo ya Kiarabu.

Kadhalika Khaji amesisitizia haja ya kufanyika duru ya sita ya mkutano wa Kamati ya Katiba ya Syria mjini Geneva, ili kusukuma mbele gurudumu la kutatuliwa mgogoro wa Syria kupitia njia za amani.

Mwanadiplomasia huyo wa Iran ameashiria hali mbaya wanayopitia wananchi wa Syria kutokana na mashinikizo na vikwazo vya nchi za Magharibi, na vile vile janga la ugonjwa wa Covid-19 na kubainisha kuwa, kuna udharura wa kuongezwa misaada ya kibinadamu kwa wanachi wa Syria.

Hali mbaya ya kibinadamu Syria

Kwa upande wake, Geir O. Pedersen, Mjumbe Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Masuala ya Syria ameshukuru na kupongeza ushirikiano wa Iran katika mchakato wa kutafutiwa ufumbuzi mgogoro wa Syria kwa njia za amani na diplomasia.

Kadhalika afisa huyo wa Umoja wa Mataifa ametoa mwito wa kupanuliwa ushirikiano wa pande mbili wa Tehrn na UN katika uwanja huo.

Tags