Aug 29, 2021 12:31 UTC
  • Mawaziri wa mambo ya nje wa Iran na Syria wakutana na kuzungumza mjini Damascus

Mawaziri wa mambo ya nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Syria wamekutana na kufanya mazungumzo katika mji mkuu wa Syria, Damascus.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian ambaye ameelekea mjini Damascus kwa safari maalum, leo amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria Faisal Miqdad.

Katika safari yake ya kwanza ya mahusiano ya pande mbili mara baada ya kuteuliwa kuwa waziri mpya wa mambo ya nje wa Iran, Amir- Abdollahian ameelekea nchini Syria leo baada ya kushiriki kikao cha kikanda cha kuiunga mkono Iraq kilichofanyika mjini Baghdad.

Mara baada ya kuwasili mjini Damascus, Amir-Abdollahian alisema, uhusiano wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na nchi mbili za Syria na Iraq ni wa kistratejia.

Katika mazungumzo yake na Faisal Miqdad, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alisema, katika safari yake ya kwanza ya mahusiano ya pande mbili akiwa waziri wa mambo ya nje ameelekea mjini Damascus na akabainisha kwamba "Iran na Syria zimechukua hatua za pamoja na kupata ushindi kwa pamoja katika medani ya kupambana na ugaidi; na akaongezea kwa kusema: "leo hii tuko hapa pamoja ili kuuangazia uhusiano wa nchi mbili katika nyanja tofauti za kibiashara, kiuchumi na nyinginezo na kufanya jitihada za kuustawisha zaidi."

Hossein Amir-Abdollahian amesema, kwa irada na utashi wa viongozi wa nchi mbili, leo Iran na Syria zitaweza kupiga hatua kubwa kwa ushirikiano wa pamoja katika uga wa kupambana na ugaidi wa kiuchumi na kuwasaidia watu wa nchi hizo mbili..../

 

Tags