Sep 08, 2021 07:12 UTC
  • Hussein Amir-Abdollahian
    Hussein Amir-Abdollahian

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Jamhuri ya Kiiislamu ya Iran ametoa wito wa kuwepo Afghanistan isiyo na vita wala ugaidi.

Hussein Amir-Abdollahian ametoa wito huo katika mazungumzo yake na rais wa zamani wa Afghanistan, Hamid Karzai, huku pande hizo mbili zikibadilishana mawazo juu ya hali ya sasa ya Afghanistan. 

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Iran amesisitiza misingi ya siasa za Jamhuri ya Kiislamu za kuwepo mazungumzo baina ya makundi na vyama vyote kwa ajili ya kuunda serikali jumuishi nchini Afghanistan ambayo itashirikisha makundi na kaumu zote za nchi hiyo. Hussein Amir-Abdollahian amesema hiyo ndiyo njia pekee ya kurejesha amani na utulivu nchini Afghanistan.

Amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeendelea kufungua mipaka yake na Afghanistan kwa ajili ya kurahisisha hali ya wananchi wa nchi hiyo na kuendeleza biashara. 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema uvamizi wa miongo miwili wa Marekani nchini Afghanistan ndiyo sababu ya hali mbaya inayoshuhudiwa sasa nchini humo.

Kwa upande wake rais wa zamani wa Afghanistan amesema viongozi wa nchi hiyo wanafanya jitihada za kuvuka kipindi cha sasa na kwamba lengo kuu ni kukidhi matakwa na mahitaji ya wananchi. 

Hamid Karzai ameishukuru Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kutokana na juhudi zake za kusaidia mchakato wa kupatikana ufumbuzi wa matatizo ya sasa ya Afghanistan na kusema: Kunafanyika mazungumzo baina ya makundi mbalimbali likiwemo kundi la Taliban na kwamba anatarajia kuwa Iran itaendelea kutoa msaada katika njia hiyo.       

Tags