Sep 10, 2021 12:53 UTC
  • Iran yalaani tuhuma za kuaibisha zilizotolewa na inayojiita kamati ya pande nne ya Jumuiya ya Waarabu

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani tuhuma za kuaibisha zilizotolewa na inayojiita kamati ya pande nne ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.

Saeed Khatibzadeh amelaani tuhuma hizo chafu zilizotolewa kupitia taarifa ya inayojiita kamati ya pande nne ya Arab League na kueleza kwamba kutolewa taarifa za aina hiyo kunaonyesha jinsi nchi za kamati hiyo zisivyo na uelewa hata mdogo wa yanayojiri katika eneo na mazingira jumla yanayotawala katika mahusiano ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na majimui ya nchi za Kiarabu.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema, kukaririwa tuhuma kwamba Iran inaingilia masuala ya nchi zingine na nchi zenye rekodi ya uingiliaji, uzushaji mivutano, kuandaa magaidi na mamluki na kuwasha moto wa vita hasa nchini Yemen na maeneo mengine yenye mapigano ya Asia Magharibi na Afrika Kaskazini, ni jambo la kupuuziliwa mbali na akaongeza kwamba, kuyakusanya pamoja mambo hayo kwa ajili ya kuituhumu Iran hakutatatua tatizo la nchi zenye hulka ya kuingilia mambo ya nchi zingine na zisizojali matakwa ya wananchi wao.

Kikao cha Jumuiya ya Nchi za Kiarabu

Khatibzadeh ameeleza kwamba, dukuduku hasa la walioandaa taarifa hiyo ni kutaka kuutumikia waziwazi na kwa kificho utawala wa Kizayuni na akaziasa nchi hizo nne kwa kuziambia, badala ya kutoa taarifa za aina hiyo zisizo na thamani, zifuatilie kwa karibu zaidi jinai zinazofanywa na utawala dhalimu wa Kizayuni wa Israel dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina.

Taarifa iliyotolewa na nchi zinazojiita kamati ya pande nne ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu imerudia tena tuhuma za kila mara dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kuituhumu kwamba inafanya uingiliaji haribifu na inawafadhili kifedha Wahouthi na makundi ya kigaidi na yenye misimamo ya kufurutu ada.../

Tags