Sep 11, 2021 01:30 UTC
  • Iran yajibu upayukaji wa waziri wa mambo ya nje wa Israel

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amejibu porojo na upayukaji wa waziri wa mambo ya nje wa utawala wa Kizayuni wa Israel na kusema kuwa, Iran ina haki ya kujibu chokochoko zozote zile.

Saeed Khatibzadeh alitoa majibu hayo jana Ijumaa kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter na kuandika: "Utawala dhalimu wa Israel usiojali sheria na ambao umejilimbikizia mabomu haramu ya atomiki na unaendelea kukaidi kujiunga na NPT, kwa mara nyingine unajipa uthubutu wa kuitishia Iran ambayo ni mwanachama wa NPT na ndiyo nchi pekee iliyofanyiwa ukaguzi mwingi na mkubwa zaidi wa mradi wake wa nyuklia kuliko nchi nyingine yoyote duniani."

"'Kijakazi huyo kipenzi' wa Magharibi amezoea kudekezwa na kubembelezwa, lakini ulimwengu hivi sasa imetambua utambulisho wake halisi wa kuvuruga amani na utulivu duniani."

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran vile vile amesema, Tehran ina haki ya kujibu chokochoko zozote inazofanyiwa.

Yair Lapid

 

Yair Lapid, waziri wa mambo ya nje wa utawala wa Kizayuni ambaye amefanya ziara mjini Moscow, Russia ameituhumu Iran kuwa eti inafanya juhudi za kumiliki silaha za atomiki.

Akizungumza na shirika la habari la Sputnik, Lapid alidai jana Ijumaa kwamba eti Iran imekaribia kumiliki silaha za nyuklia na ielewe kuwa jambo hilo haliwezi kuachwa vivi hivi na Israel.

Juzi Alkhamisi pia, waziri wa mambo ya nje wa utawala wa Kizayuni alifanya mazungumzo na waandishi wa habari akiwa pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Sergey Lavrov na kudai kuwa, Israel haiwezi kuiruhusu Iran kumiliki eti silaha za nyuklia.

Tags