Sep 16, 2021 09:01 UTC
  • Safari ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Tajikistan; umuhimu na malengo yake

Sayyid Ibrahim Raisi, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Alkhamisi ya leo ameelekea Dushanbe, mji mkuu wa Tajikistan kwa ajili ya kushiriki na kuhutubia mkutano wa wakuu wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai unaofanyika nchini humo leo na kesho.

Rais Ibrahim Raisi ambaye hii ni safari yake ya kwanza nje ya nchi tangu alipochukua madaraka ya nchi baada ya kushinda uchaguzi wa Rais wa Juni mwaka huu, ameelekea Tajikistan akiitikia mwaliko wa Rais wa nchi hiyo Emomali Rahmon. Katika safari hiyo mbali na kuhutubia katika mkutano wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai, (The Shanghai Cooperation Organization (SCO), Rais wa Iran atakutana na kufanya mazungumzo pia pambizoni mwa mkutano huo na viongozi wa mataifa mbalimbali wanaoshiriki katika mkutano huo. Adha Rais Ibrahim Raeisi atakuwa na mazungumzo ya pande mbili pia na mwenyeji wake Rais Emomali Rahmon. Safari hii ya kwanza ya Ayatullah Raisi nje ya nchi tangu alipoapishwa na kuanza kuongoza rasmi ina umuhimu kutokana na sababu kuu mbili.

Sababu ya Kwanza; ni mwaliko rasmi wa Rais wa Tajikistan na mazungumzo ya pande mbili na viongozi wa nchi ambayo ina uhusiano mkongwe na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Kuweko ujumbe wa ngazi ya juu wa viongozi wa kisiasa na kiuchumi walioandamana na Rais wa Iran katika safari hiyo, wakiwemo Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni, Nishati, Kazi na Ustawi wa Jamii, Sheria na Turathi za Kiutamaduni kunaonyesha kuzingatia malengo ya pande mbili katika uhusiano na mazungumzo kuhusiana na ushirikiano mpya ambao unapewa kipaumbele na serikali ya awamu ya 13 ya Iran katika sera na diplomasia yake ya kieneo.

Sababu ya Pili; ni kwamba, kushiriki Rais wa Iran katika mkutano wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai kama mwanachama mtazamaji na kuhutubia katika mkutano huo, bila shaka kunaambatana na mitazamo na malengo ya pande mbili na pande kadhaa na kubainisha misimamo ya Tehran kuhusiana na amani na uthabiti wa eneo la Asia Magharibi hususan hali ya sasa ya Afghanistan na masuala mengine ya kieneo na kimataifa.

Kwa mtazamo huo, safari ya kwanza ya Rais Ibrahim Raisi nje ya nchi huko Tajikistan na kushiriki kwake katika mkutano wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai inabeba risala na jumbe kadhaa maalumu.

Kuundwa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai licha ya kuwa kunarejea nyuma takribani miongo miwili iliyopita, lakini jumuiya hii hivi sasa inahesabiwa kuwa kiigizo kipya cha eneo barani Asia kutokana na kuwa na nchi muhimu za eneo hili ambazo ni wanachama wa jumuiya hiyo. Mataifa makubwa kama Russia na China ambayo ni wanachama wenye taathira muhimu katika Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai yana uhusiano mzuri na wa kistratijia na Iran ambayo kwa sasa ni mwanachama mtazamaji katika jumuiya hiyo.

Katika kutathmini umuhimu wa ushirikiano wa Iran na Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai weledi wa masuala ya Asia ya Kati na Caucasia wanaashiria nyuga mbalimbali kama za nishati, usafiri na uchukuzi na kusema, nyanja hizi zina umuhimu wa kistratijia katika eneo.

Katika jiografia ya kieneo ya Shanghai, uhusiano wa kibiashara katika maji huru na ya kimataifa na upitiaji wa bidhaa zinazosafirishwa kuelekea mataifa mengine ni jambo lenye umuhimu mkubwa ambapo hilo linawezekana kwa kutumia njia za Iran ambazo ni rahisi kupitika. Hasa kwa kutilia maanani kwamba, Iran ina njia muhimu kabisa za mawasiliano katika eneo la Asia Magharibi. Kuhusiana na hilo tunaweza kuashiria njia muhimu kama bandari ya kistratijia ya Chabahar na njia za reli na barabara ambazo zinaweza kutumiwa kuifikia bandari hiyo kupitia njia ya ya mashariki mwa Asia na kuiunganisha na Asia ya Kati na Magharibi, ambapo hii inahesabiwa kuwa ni fursa isiyo na mithili kwa ajili ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai (SCO).  

Muda mchache kabla ya Rais Ibrahim Raeisi kuondoka Tehran kwa ajili ya kuelekea Tajikistan

Kwa upande wa usalama wa wote katika eneo, pia tunapaswa kusema kuwa, kwa kuzingatia malengo ya Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai ambayo yamejengeka juu ya msingi wa mitazamo ya pande kadhaa, ushirikiano wa Iran na jumuiya hiyo unaendana na mitazamo ya pamoja ya kieneo na ya pande kadhaa.

Matukio ya muongo mmoja uliopita katika eneo yamethibitisha nafasi na mchango wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika ushirikiano wake wa kistratijia na Russia kwa minajili ya kupambana na ugaidi nchini Syria na kulinda maslahi ya pamoja katika kukabiliana na vitisho vya pamoja, ambapo jambo hili lina umuhimu mkubwa na maalumu kwa jumuiya ya Shanghai.

Stratijia ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya ushirikiano wa kieneo ni kukuza na kuimarisha mahusiano ya kisiasa na ushirikiano wa kiusalama, kiuchumi, kibiashara na kiutamaduni na kupanua ushirikiano wa muelekeo wa pande kadhaa kwa minajili ya kukabiliana na mtazamo wa upande mmoja wa ulimwengu wa Magharibi. Kwa kuzingatia yote haya tunaweza kusema kuwa, sababu za Iran kuwa na hamu na shauku ya kushirikiana na Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai ni kutilia mkazo nukta zilizoashiriwa na kuanzisha uwezo mpya kwa ajili ya ushirikiano wa pande kadhaa na hivyo kudhamini maslahi ya kila upande. Umuhimu wa safari ya Rais Ibrahim Raisi nchini Tajikistan na kushiriki kwake katika mkutano wa viongozi wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai (The Shanghai Cooperation Organization (SCO) unatathminiwa katika kalibu hii.