Sep 17, 2021 11:29 UTC
  • Rais Ibrahim Raeisi: Jumuiya ya Shanghai inaweza kuwa kichocheo cha mtazamo mmoja wa pande kadhaa

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai (SCO) inaweza kuwa kichocheo muhimu cha mtazamo mmoja wa pande kadhaa ulimwenguni.

Rais Ibrahim Raeisi amesema hayo katika hotuba yake kwenye mkutano wa 21 wa wakuu wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai huko Dushanbe mji mkuu wa Tajikistan na kueleza kwamba, jumuiya hiyo imeonyesha vizuri kwamba, inaweza kugeuka na kuwa tegermeo la kiuchumi na kisiasa katika mtazamo mmoja na ushirikiano wa kadhaa ulimwenguni.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, sera za kigeni za Tehran siku zote zimejikita katika ushiriki amilifu katika asasi na jumuiya za kimataifa, mitazamo ya pande kadhaa na kupinga uchukuaji maamuzi wa upande mmoja.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akihutubia katika mkutano wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai (SCO)

 

Aidha Sayyid Ibrahim Raeisi amesema katika hotuba yake hiyo kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikitilia mkazo suala la ushirikiano uliojengeka katika msingi wa kuheshimiana na udharura wa kuweko mchango wenye kujenga kwa minajili ya kukabiliana na changamoto za kieneo na kimataifa.

Mkutano wa siku mbili wa wakuu wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai ulianza Alkhamisi ya jana katika mji mkuu wa Tajikistan Dushanbe, ambapo Rais Ibrahim Raeisi ameuongoza ujumbe wa ngazi za juu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mkutano huo, hii ikiwa ni safari yake ya kwanza nje ya nchi tangu alipoapishwa na kuchukua rasmi madaraka ya nchi akimrithi Rais aliyepita Hassan Rouhani.