Sep 19, 2021 12:23 UTC
  • Mafanikio ya kiistratijia ya kutumwa mafuta ya Iran nchini Lebanon; nguvu za muqawama za kutatua mgogoro

Malori ya kwanza ya mafuta ya Iran yaliwasili nchini Lebanon Alkhamisi tarehe 16 Septemba, 2021 na kupokewa kwa shauku na furaha kubwa na wananchi wa nchi hiyo. Shehena ya pili ya mafuta hayo iliwasili Jumamosi asubuhi, Septemba 18 baada ya kuvuuka mpaka wa Syria na kuingia Lebanon.

Hatua ya kutumwa mafuta ya Iran nchini Libenon ni jambo ambalo hata wapinzani wanakiri kuwa ni ushindi mkubwa kwa Iran na Hizbullah ya Lebanon, hata kama hawatangazi hadharani. Kuna sababu mbalimbali zinazofanya kila mmoja akiri kwamba huo ni ushindi mkubwa wa kiistratijia.

Mosi: Meli ya kwanza ya mafuta ya Iran kwa ajili ya wananchi wa Lebanon ilifikia kwenye bandari ya Baniyas ya Syria baada ya kukata masafa marefu ya bahari kubwa, mfereji wa Suez na baadaye kupelekwa Lebanon. Mafuta hayo yamefikishwa salama usalimini nchini Lebanon kutokana na nguvu za kiulinzi wa Iran na Hizbullah, lakini pia yameweza kuwakwamua na kuwaokoa wananchi wa Lebanon waliokuwa wanateseka kwa vikwazo vya kidhalimu vya Marekani.

Pili: Kufanikiwa Iran kufikisha mafuta nchini Lebanon, ni uthibitisho mwingine juu ya uwezo wa Iran na Hizbullah wa kumfanya adui asithubutu kucheza na kambi ya muqawama. Sayyid Hasan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon alikuwa ametangaza kuwa, Meli za Iran zilizobeba mafuta ya Lebanon, ni sawa na ardhi ya Lebanon, kuanzia zilipoanza safari hadi kuwasili kwake na kwamba jaribio lolote la kuhatarisha usalama wa meli hizo litapata majibu makali kutoka kwa Hizbullah. Msimamo huo imara na usiotetereka wa Sayyid Hasan Nasrullah uliwatia woga hata Wazayuni na hawakuthubutu kuzifanyia meli za Iran usumbufu wowote ule.

Msafara wa malori ya mafuta ya Iran nchini Lebanon

 

Tatu: Jambo lililo muhimu ni kuwa, watu wengi wanaamini kwamba kufanikiwa Iran kufikisha mafuta yake nchini Lebanon kwa usalama kamili na bila ya usumbufu wowote, ni pigo kubwa kwa Marekani na vibaraka wake wa Asia Magharibi. Sababu yake ni kuwa, mafuta hayo yamepelekea kuvunjika siasa za vikwazo na kuizingira Lebanon pamoja na Iran. Marekani na vibaraka wake hasa nchi za Kiarabu zilifanya njama kubwa za vikwazo vya mafuta ili kuitumbukiza Lebanon katika mgogoro na ugomvi wa kisiasa na kuituhumu Hizbullah kuwa ndiyo inayosababisha matatizo hayo. Sasa hivi si tu Hizbullah haituhumiwi tena kuhusika na mgogoro wa mafuta, lakini pia nafasi ya harakati hiyo ya Kiislamu imeimarika zaidi kutokana na ubunifu wa Sayyid Hasan Nasrullah wa kutatua mgogoro wa mafuta wa Lebanon. 

Ni vyema tukumbushe hapa kwamba, Waziri wa Kazi wa serikali mpya ya Lebanon Muṣṭafá Bayram alisema siku ya Alkhamisi sambamba na kuingia misafara ya mafuta ya Iran katika ardhi ya nchi hiyo kwamba, mafuta hayo yamevunja mzingiro wa kihistoria na wa kidhalimu ambao Marekani ilikuwa imeiwekea Lebanon.

Gebran Bassil, Waziri wa Mambo ya Nje wa zamani wa Lebanon

 

Naye Gebran Bassil, Waziri wa Mambo ya Nje wa zamani wa Lebanon ambaye ni mkuu wa chama cha Mrengo wa Kitaifa wa Ukombozi wa Lebanon alisema kuhusu kuingia misafara ya mafuta ya Iran nchini humo kutokea Syria kwamba wakati maadui wa taifa na wananchi wa Lebanon walipofanya njama za kuwatesa wananchi hao kwa kuwanyima mafuta, wananchi hao walikuwa na haki ya kudhamini mahitaji yao ya bidhaa hiyo muhimu kutoka sehemu yoyote ile.

Nne: Hatua ya Iran ya kuwafikishia mafuta wananchi wa Lebanon, imekwenda sambamba na kuzuka suala la Afghanistan na hali yake mbaya waliyosababishiwa wananchi wa Afghanistan na dola la kibeberu la Marekani. Kutokea kwa wakati mmoja masuala hayo mawili kuna umuhimu wa aina mbili. Mosi ni kwamba imethibitika kivitendo kuwa Marekani haiguswi na wala haishughulishwi na usalama wa hata marafiki zake. Pili ni kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeshikamana vilivyo na waitifaki wake, na mara zote ni mwaminifu kwao. Ni kwa sababu hiyo ndio maana Nasir al Shammari, Msemaji Rasmi wa Muqawama wa Kiislamu wa Harakati ya al Nujaba ya Iraq akasema kuwa, hatua ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya kuwafikishia mafuta wananchi wa Lebanon imethibitisha kwa mara nyingine kuwa Iran ni mkweli katika ahadi zake na kamwe haiwaachi mkono waitifaki wake, na haya ni mafanikio mapya ya kiistratijia kwa wananchi na muqawama wa Lebanon. 

Tags