Sep 21, 2021 12:17 UTC
  • Iran yajibu madai ya ovyo ya Saudia, yaonya kuhusu usiri wa miradi ya nyuklia ya Riyadh

Mwakilishi wa Iran amejibu madai ya uongo na ya ovyo ya waziri wa nishati wa Saudi Arabia aliyotoa kwenye mkutano mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA na kusema kuwa, Saudia ndio kwanza inaheshimu sehemu ndogo to ya nakala ya zamani ya protokali za nyuklia lakini pamoja na hayo inajipa uthubutu wa kusimama mbele ya watu na kuwatuhumu wengine kuhusu miradi yao ya nyuklia.

Khudayar Rouzbahani, mwakilishi wa kisiasa na mjumbe wa kudumu wa Iran katika Taasisi za Kimataifa zenye makao yao mjini Vienna amewaambia waandishi wa habari kwamba, Iran inaheshimu kikamilifu na kiukweli mkataba mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA na inaamini kwa dhati kwamba  kuachwa kutekelezwa mkataba huo ni kengele ya hatari  popote pale, ni sawa aliyefanya hivyo ni Saudi Arabia au utawala wa Kizayuni; ubaguzi wowote ule haukubaliki katika suala hilo. Amesema: Kuvunja mkataba huo mkuu wa IAEA ni jambo la hatari sana na inabidi jambo hilo liachwe mara moja bila ya taasubu wala ubaguzi wowote.

Mwanadiplomasia hiyo wa Iran ameongeza kuwa, Tehran, wakala wa IAEA na jamii ya kimataifa zitafurahi sana kama Saudia na wengine Mashariki ya Kati wataheshimu na kutekeleza mkataba huo wa IAEA unaotekelezwa kikamilifu hivi sasa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Shughuli za nyuklia za Saudi Arabia zisizosimamiwa na sheria za kimataifa

 

Ameongeza kuwa, inasikitisha kuona kuwa, ukaidi wa baadhi ya nchi wa kutokubali kuwa wanachama wa Mkataba wa Kimataifa wa Kuzuia Uenezaji na Uzalishaji wa Silaha za Atomiki NPT unafanywa kisingizio na nchi hizo cha kukwepa kutekeleza majukumu yao ya kuondoa wasiwasi wa walimwengu kuhusu shughuli zao za nyuklia. 

Amesema, mara chungu nzima wakala wa IAEA umeitaka Saudi Arabia iwe muwazi katika shughuli zake za nyuklia lakini Riyadh inafanya ukaidi na hivi sasa inajipa uthubutu wa kuwatuhumu wengine kuhusu miradi ya nyuklia.