Sep 23, 2021 11:25 UTC
  • Iran: Jeshi letu la majini linaweza kufika popote linapohitajika ulimwenguni

Kamanda wa Kikosi cha Majini cha Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, vyombo vya majini vya jeshi hilo vina uwezo wa kufika katika nukta na sehemu yoyote inayohitajika duniani.

Admiral Shahram Irani amesema hayo katika mahojiano na televisheni ya al Alam na kusema kuwa, msafara wa 75 wa vyombo vya majini vya Iran umekata masafa ya kilomita 45,000 katika operesheni yake ya siku 133 na kufanikiwa kuvuka Bahari Kuu tatu na kupita kwenye fukwe za nchi 55 rafiki na maadui bila ya hata kutia nanga.

Admiral Irani ameongeza kuwa, maadui wa Iran hawakufurahishwa na mafanikio hayo ya msafara mkubwa wa baharini wa Jamhuri ya Kiislamu, lakini mwisho wamelazimika kuheshimu azma na nia ya kweli ya wananchi wa Iran. 

Sherehe za kuwapongeza wanamaji wa Iran kwa kuweza kuendesha operesheni hiyo kwa mafanikio makubwa. Ujumbe wa maandishi kwenye picha unasema: TUMEWEZA...

 

Kamanda huyo wa Kikosi cha Majini cha Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia amesema, ujumbe wa operesheni hiyo ni kwamba, Iran inaweza kufika katika nukta na eneo lolote lile duniani inapohitajika kufanya hivyo na ina uwezo wa kulinda usalama wa eneo hili bila ya kutegemea madola baki yasiyo na uhusiano wowote na eneo hili.

Tarehe 9 mwezi huu wa Septemba 2021, msafara huo wa 75 wa vyombo vya Kikosi cha Majini cha Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran  ulirejea humu nchini baada ya kukata masafa ya kilomita 45,000 kwa muda wa siku 133 bila ya kutia nanga katika bandari yoyote ile ya nje ya Iran.

Moja ya malengo ya safari hiyo ni kuonesha nguvu za Kikosi cha Majini cha Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa mataifa rafiki na adui.