Sep 25, 2021 02:33 UTC
  • Sisitizo la Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran juu ya Umoja wa Mataifa kuimarisha nafasi yake katika utatuzi wa migogoro ya kimataifa

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaunga mkono ubunifu wa Umoja wa Mataifa katika kusaidia kurudisha amani na usalama wa kimataifa na wakati huo huo kukaribisha misimamo ya Katibu Mkuu wa umoja huo isiyopendelea upande wowote na ya kiadilifu katika uwanja huo.

Hayo yamesemwa na Hussein Amir Abdollahiyan, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alipokutana na kuzungumza na Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, pembeni mwa kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York.

Amir Abdollahiyan amesema Umoja wa Mataifa unapasa kuwa na nafasi kubwa zaidi na ya kiadilifu katika utatuzi wa migogoro inayoendelea katika nchi za Palestina, Yemen, Syria na Afghanistan. Amesema Palestina hivi sasa inakabiliwa na hali mbaya na ya kusikitisha ya kibinadamu kutokana na hatua za kijinai ambazo zimekuwa zikitekelezwa kwa miongo kadhaa na utawala haramu wa Israel katika ardhi hizo zinazokaliwa kwa mabavu. Amesisitiza kwamba njia pekee ya kutatuliwa mgogoro wa ardhi hizo ni kufanyika kura ya maoni itakayowashirikisha wakazi wote asilia na wazalendo wa nchi hiyo. Amir Abdollahiyan amesikitishwa na utendaji dhaifu wa Umoja wa Mataifa katika miaka iliyopita na kutumai kwamba hali hiyo itarekebishwa kutokana na uongozi wa Guterres.

Ukweli wa mambo ni kuwa katika miongo kadhaa iliyopita, masuala mawili muhimu yametawala ulimwengu nayo ni ya ukaliaji kimabavu ardhi za mataifa mengine na ugaidi. Ni wazi kuwa kuendelea kwa suala hilo kutakuwa na athari mbaya na hatari kwa usalama wa ulimwengu. Iran ni moja ya nchi ambazo zimekuwa wahanga wakuu wa vikwazo na ugaidi wa Marekani. Kuuawa kigaidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) ambaye alikuwa na mchango mkubwa katika kuangamiza kundi la kigaidi la Daesh katika Mashariki ya Kati ni mfano wa wazi katika uwanja huo.

Hussein Amir Abdollahiyan (kushoto) akiwa na Antonio Guterres mjini New York

Luteni Jenerali Qassem Soleimani, ambaye alikuwa safari nchini Iraq kufuatia mwaliko rasmi wa viongozi wa nchi hiyo, aliuawa kigaidi tarehe 3 Januari 2020 kwa amri ya Donald Trump rais wa wakati huo wa Marekani. Aliuawa shahidi akiwa na Abu Mahdi al Muhandis, Naibu Kamanda wa Kikosi cha Kujitolea cha Wananchi wa Iraq (Hashd al Shaabi) na wanapambano wengine wanane katika shambulio la anga lililotekelezwa na askari vamizi wa Marekani karibu na uwanja wa ndege wa Baghdad. Shahid Qassem Soleimani alikuwa mwanastratijia mashuhuri wa kijeshi na ambaye alifichua madai ya uongo ya Marekani kuhusiana na suala zima la mapambano dhidi ya ugaidi wa kimataifa. Mapambano yake katika uwanja huo yalivunja njama zote zilizofanywa na Marekani na mshirika wake mkuu katika eneo, utawala ghasibu wa Israel, kwa ajili ya kutaka kuligawa eneo hili katika mapande madogo madogo ya ardhi.

Kama alivyosema Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Shahid Soleimani aliushinda ubeberu katika hali zote mbili za uhai na kuuawa kwake shahidi.

Huku akiashiria matamshi ya rais wa Marekani aliyesema kuwa licha ya nchi hiyo kutumia dola trilioni 7 katika eneo lakini hakuna faida yoyote iliyoipata, Ayatullah Khamene amesema shujaa wa kazi hiyo kubwa ni Luteni Soleimani, ambayo aliifanya katika uhai wake.

Bila shaka  siasa za upande mmoja za Marekani na uungaji mkono wake kwa ugaidi pamoja na fikra za kupindukia mipka na vilevile upuuzaji wake wa sheria za kimataifa na wakati huo huo uzembe wa Umoja wa Mataifa katika kutekeleza majukumu yake ya kulinda amani na usalama duniani ni mambo ambayo yameligeuza eneo la Asia Magharibi kuwa kituo cha migogoro na ghasia. Matukio ya kusikitisha ambayo yametokea katika nchi za Iraq, Syria, Afghanistan na Yemen katika miongo ya karibuni yamethibitisha wazi kuwa mataifa ya eneo yamekuwa mhanga mkuu wa siasa za uchokozi na  ugaidi unaoungwa mkono na Marekani.

Wakati huo huo Marekani inatekeleza siasa za jinai dhidi ya binadamu kwa kuendeleza vikwazo vya kidhalimu dhidi ya taifa la Iran ambapo hata imezuia watu wa nchi hii kufikishiwa dawa na bidhaa za dharura za afya tena katika kipindi hiki kigumu cha kuenea duniani virusi hatari vya corona. Ni wazi kuwa Marekani inapasa kuwajibishwa na jamii ya kimataifa kuhusu suala hilo.

Marekani inatumia vikwazo kama wenzo wa kuyashinikiza mataifa pinzani

Matukio hayo yanathibitisha kuwa hatima ya mataifa yote ni moja. Usalama, ugaidi, uchumi na mapambano dhidi ya corona ni masuala ambayo yanahitajia ushirikiano wa mataifa yote  katika kivuli cha usimamizi wa Umoja wa Mataifa ili kuweza kuyatatua. Umoja wa Mataifa na Baraza Kuu lake, ni fursa kwa ajili ya kubainishwa fikra na mawazo ya mataifa mbalimbali kwa ajili ya kukabiliana na changamoto na matarajio kutoka kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kukabiliana na mambo yanayotishia usalama wa dunia.