Sep 25, 2021 02:36 UTC
  • Ebrahim Raisi: Ni jambo la dharura kustawishwa mauzo ya bidhaa za Iran kwa Iraq na nchi jirani

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, ni jambo la dharura kustawishwa uuzaji wa bidhaa za Iran kwa Iraq na nchi jirani na inabidi miundombinu ya kufanikisha jukumu hilo iimarishwe kadiri inavyowezekana.

Sayyid Ebrahim Raisi alisema hayo jana (Ijumaa) na kuongeza kuwa, si sahihi kiwango cha usafirishaji bidhaa za Iran kwa nchi jirani kiwe ni asilimia 2 tu, bali kuna wajibu idadi ya bidhaa hizo ziongezwe kutoka dola bilioni 20 hadi bilioni 40 au 50 kupitia hatua za haraka, za dharura na kufanya kazi kijihadi.

Rais Raisi amegusia jinsi Iran ilivyo na mpaka mrefu wa kilomita 430 na Iraq huko Ilam (magharibi mwa Iran) na kusisitiza kuwa, mpaka wa nchi na nchi si tishio, bali ni fursa nzuri ya kuwaunganisha watu wa nchi mbili za Iran na Iraq hasa wakazi wa mkoa wa Ilam ambao wana historia pana, kubwa na ndefu ya pamoja ya kiitikadi, kiutamaduni na kidini. 

Rais Ebrahim Raisi katika mazungumzo na wananchi wa mkoa wa Ilam wa magharibi mwa Iran

 

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vile vile ametaka kuundwe jopo kazi la kisheria na kiuchumi baina ya nchi mbili za Iran na Iraq katika mkoa wa Ilam na maeneo ya Iraq yanayopakana na mkoa huo kwa ajili ya kuondoa matatizo ya usafirishaji bidhaa na kuongeza kiwango cha mabadilishano ya kibiashara baina ya pande mbili.

Jana asubuhi, Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliwasili mkoani Ilam (magharibi mwa Iran), ikiwa ni muendelezo wa ziara zake za kikazi katika maeneo tofauti humu nchini na ameonana na maulamaa, watu wenye vipaji na familia za mashahidi na watu wanaojitolea katika njia ya haki wa mkoa huo.