Sep 26, 2021 15:08 UTC
  • Raisi: Vikwazo haviwezi kuzuia kustawisha uhusiano kati ya Iran na nchi nyingine

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, vikwazo haviwezi kuzuia kustawisha uhusiano na ushirikiano wa Iran na nchi nyingine.

Rais Sayyid Ebrahim Raisi ameashiria uhusiano mzuri wa Iran na Austria na kusema: Iran iko tayari kikamilifu kustawisha ushirikiano wa kibiashara na Austria na nchi nyingine na kwamba vikwazo na vizuizi kamwe haviwezi kuzizuia nchi mbili katika uwanja huo. Rais wa Iran ameeleza hayo leo hapa Tehran baada ya kupokea hati ya utambulisho za Wolf  Dietrich Heim, balozi mpya wa Austria hapa nchini.  

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amevitaja vikwazo dhidi ya Iran kuwa ni kinyume cha sheria na vya kidhalimu na kueleza kuwa: Kwa kuzingatia ripoti nyingi zilizotolewa na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) kwamba miradi ya nyuklia ya Iran ina malengo ya amani, kitendo cha kuiweka Tehran vikwazo hakina msingi wowote hasa ikitiliwa maanani kuwa, Iran imetekeleza ahadi na majukumu yake yote ndani ya mapatano ya JCPOA, ilhali viongozi wa Marekani ambao walijitoa kwa upande mmoja katika mapatano hayo na nchi za Ulaya hazijatekeleza mapatano hayo. 

Rais Raisi ameashiria pia shukran zilizotolewa na balozi wa Austria kwa Iran kutokana na kuwapokea wakimbizi wa Kiafghani na kuongeza kuwa: Kiteno cha wananchi wa Afghanistan kuwa wakimbizi ni matokeo ya miongo miwili ya siasa na hatua za Marekani nchini humo; na sisi tumekuwa wenyeji wa wahajiri wa Kiafghani kutokana na mtazamo wa ubinadamu na Uislamu.  

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa, nchi za Ulaya zinapaswa kutekeleza majukumu yao hasa kwa kuzingatia mamilioni ya wakimbizi wa Afghanistan walioko nchini Iran. Vilevile ameitaka Austria kuwasilisha suala hilo kwa nchi hizo za Ulaya.  

Kwa upande wake balozi mpya wa Austria mjini Tehran ameashiria  uhusiano mwema wa nchi yake na Iran na kuongeza kuwa: Austria inataka kuimarishwa uhusiano wa nchi mbili hizi hususan katika uga wa mabadilishano ya kiuchumi. Wolf Dietrich Heim amesema kuwa: Iran na Austria zimeweza kufanikisha baadhi ya miradi katika kipindi cha vikwazo. 

Balozi mpya wa Austria akikabidhi hati yake ya utambulisho kwa Rais wa Iran