Sep 27, 2021 13:32 UTC
  • Hossein Amir Abdollahian
    Hossein Amir Abdollahian

Kabla ya kurejea nchini wiki hii akitokea Marekani, Hossein Amir Abdollahian Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alieleza kwamba: "Jumbe zinazokinzana tunazotumiwa na viongozi wa Marekani kupitia vyombo vya habari au duru za kidiplomasia hazitakuwa kigezo cha sisi kuchukua maamuzi ya mwisho."

Awali pia Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alikuwa na mazungumzo huko New York na Mkuu wa Siasa za Nje wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell ambapo alisema: Tunachunguza kwa umakini rekodi ya mazungumzo yaliyopita, na serikali mpya itaanza tena mazungumzo hayo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alisema: Kigezo chetu ni matendo ya upande wa pili na si matamshi yao. Serikali mpya ya Tehran inapitia na kuchunguza kwa makini mazungumzo yaliyofanyika hadi sasa. Haipotezi muda na wala haiafiki hatua zisizojenga za Marekani na haina lengo la kukwamisha nchi kwa ahadi tupu. Matamshi hayo ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran kuhusu mapatano ya JCPOA na kuanza tena mazungumzo huko Vienna yana nukta mbili muhimu. 

Kwanza ni swali kuwa, je Marekani ina nia ya dhati ya kurejea katika mapatano ya JCPOA na kutekeleza ahadi na majukumu yake? Hivi sasa kuna shaka nyingi kuhusu suala hilo, kwa sababu kivitendo,  hakuna kilichotokea isipokuwa sehemu ndogo sana ya ahadi za Marekani na Ulaya tena katika kipindi makhsusi. Hii ni pamoja na kuwa, nyendo za Marekani katika mapatano ya JCPOA zinakinzana. Kwa upande mmoja inatoa wito wa kurejea katika mapatano ya JCPOA na katika upande mwingine inaiwekea Iran vikwazo vipya. 

Mapatano ya JCPOA yaliyopasishwa na Baraza la Usalama la UN 

Nukta ya pili katika matamshi ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ni jibu lenye maana kwa nchi za Ulaya ambazo zinatumia mashinikizo dhidi ya Iran kutaka kutekeleza kwa upande mmoja mapatano ya JCPOA bila kujali mienendo ya Marekani ya kupuuza utekelezaji wa ahadi na majukumu yake na kwa kufumbia macho sababu zinazoifanya Iran isiiamini nchi hiyo. Kama kweli Marekani ilikuwa na wasiwasi wa kupoteza muda kwa madhara ya mapatano ya JCPOA basi ingeheshimu na kutekeleza majukumu yake na hivyo kuzuia kujitokeza mazingira ya sasa. Tajiriba inaonyesha kuwa, hakika ya hatua za kidiplomasia za Marekani inaweza kuchambuliwa na kujulikana vyema kwa kutazama kwa makini sera kuu ya serikali ya Washington mkabala na Iran.  

Joe Biden alisema katika mahojiano na gazeti la New York Times wakati akianza kazi kama Rais wa Marekani kwamba: "Kwa kushauriana na waitifaki na washirika wetu tunakusudia kuingia kwenye mazungumzo na kufikia mapatano ya baadaye ili kuimarisha na kurefusha vizuizi vya nyuklia dhidi ya Iran na kufuatilia miradi ya makombora ya nchi hiyo."  

Rais Joe Biden wa Marekani  

Hayes Brown mwandishi ina mchambuzi wa masuala ya uhusiano wa kimataifa ameashiria siasa zisizo na mantiki za Washington kuhusu mapatano ya JCPOA na kusema: "Mienendo ya Marekani ni mzaha na maskhara, kwa sababu ni sisi (Wamarekani) tulioanza kujitoa katika mapatano ya JCPOA. Wanadiplomasia wa Marekani hawawezi kukwepa ukweli kwamba, hali ya sasa imesababishwa na Marekani. Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) hadi kufikia mwaka 2018 ulikuwa imethibitisha mara kadhaa kuwa Iran imefungamana na kuheshimu vipengee vya mapatano hayo. Hakukuwepo jambo lolote la kuhalalisha kujitoa katika mapatano hayo ghairi ya kwamba, tunapenda makuu, na suala hili linakinzana na msingi wa mazungumzo yenye nia njema." 

Ni dhahir shahir kuwa siasa za Marekani mkabala wa Iran ni mwendelezo wa sera za nchi hiyo za kuiwekea Iran mashinikizo ya kiuchumi ya kiwango cha juu. Kwa maana kuwa, Marekani inataka kuilazimisha Iran eti irejee kwenye mapatano ya JCPOA na kufanya mazungumzo kuhusu kadhia nyinginezo kwa kustafidi na diplomasia na sambamba na kudumisha vikwazo. 

Ni kwa sababu hiyo ndipo Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran akasema kuwa ili kuweza kujua nani mkosa, kuna udharura wa kuelekeza macho katika miji mikuu ya Ulaya na Marekani na si Tehran, na kusisitiza kuwa kigezo cha Iran ni matendo na mienendo ya Marekani.