Oct 01, 2021 13:32 UTC
  • Kamanda wa jeshi la nchi kavu la Iran: Tunazifuatilia kikamilifu harakati za Wazayuni

Kamanda wa vikosi vya nchi kavu vya Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa tangu uje utawala wa Kizayuni karibu na mipaka ya nchi, Iran imezidi kuguswa na suala la usalama wa mpaka wake wa kaskazini magharibi na kwa sababu hiyo harakati za utawala huo haramu zinafuatiliwa kikamilifu.

Brigedia Jenerali Kioumars Heydari, ameyasema hayo leo sambamba na kuanza kwa luteka iliyopewa jina la "Wakomboaji wa Khaybar" inayofanyika katika maeneo ya kaskazini magharibi mwa Iran na kuongeza kwamba, katika karne mbili za karibuni, Jamhuri ya Kiislamu na Iran azizi haijawahi kufanya uvamizi dhidi ya yeyote na wala kuonyesha uchu na tamaa kwa ardhi ya majirani zake, bali ilichofanya ni kujilinda na kujihami tu.

 Heydari amesema, "katika eneo hili tuna mvurugaji wa amani asiyetakikana kuwepo, ambaye amekuja kutokea mahali kwingine, naye ni utawala haramu wa Kizayuni; na tangu utawala huu ulipokuja, tumezidi kuguswa na usalama wa mpaka huu, na tunafuatilia harakati zake kikamilifu."

Kamanda wa vikosi vya nchi kavu vya jeshi vilevile amesema, mbali na maudhui hizo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran bado haijathibitikiwa kwamba magaidi waliotokea Syria na kupiga kambi katika eneo hilo la mpaka wa kaskazini magharibi wameshaondoka; na kwa sababu hiyo Iran iko hasasi na inaguswa na suala hilo pia.

Mazoezi ya kijeshi ya "Wakomboaji wa Khaybar" ya Jeshi la Nchi Kavu la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yameanza leo katika eneo la umma la kaskazini magharibi mwa nchi kwa kushirikisha divisheni kadhaa, zikiwemo za mizinga, ndege zisizo na rubani na helikopta za vikosi vya anga.../

Tags