Oct 08, 2021 00:56 UTC
  • Iran na Lebanon zasisitizia haja ya kuimarisha uhusiano wa pande mbili

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu itaendelea kuliunga mkono na kulisaidia taifa la Lebanon linalokabiliwa na mgogoro wa kiuchumi uliotokana na vikwazo.

Hossein Amir-Abdollahian alisema hayo jana Alkhamisi katika mazungumzo yake na Michel Aoun, Rais wa Lebanon mjini Beirut, ambapo pia amesisitiza juu ya haja ya kuimarisha uhusiano wa pande mbili katika nyanja tofauti za kieneo na kimataifa.

Amir-Abdollahian ameeleza bayana kuwa, Iran iko tayari kuisaidia Lebanon katika kufanikisha miradi yake mbalimbali ya ustawi, hususan katika uga wa nishati. 

Kwa upande wake, Rais Michel Aoun wa Lebanon amesema wananchi na maafisa wa serikali ya nchi hiyo wanaitazama Iran kama nchi rafiki, na wanaipongeza kwa kulipa taifa hilo la Kiarabu misaada isiyo na kifani.

Ameashiria pia kuhusu umuhimu wa mazungumzo yanayoendelea kati ya Iran na Saudi Arabia na kubainisha kuwa, "Beirut inafurahishwa na uhusiano wa karibu wa Tehran na nchi za eneo, wenye lengo la kuimarisha amani ya kanda. Mazungumzo kama haya yanaweza kuyaleta pamoja mitazamo tofauti katika masuala yenye utata."

Amir-Abdollahian (kushoto) na Nabih Berri, Spika wa Bunge la Lebanon

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran amesisitiza kuwa, ziara yake nchini Lebanon inaashiria uhusiano uliokita mizizi na wa kirafiki baina ya Tehran na Beirut, na kwamba Jamhuri ya Kiislamu itaendelea kuwaunga mkono wananchi, jeshi na kambi ya muqawama katika nchi hiyo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran hapo jana alikutana pia na kufanya mazungumzo na Nabih Berri, Spika wa Bunge la Lebanon, Waziri Mkuu, Najib Mikati na Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo ya Kiarabu, Abdullah Bou Habib.

Tags