Oct 10, 2021 07:52 UTC
  • Iran: Tutaendelea kuiunga mkono kambi ya muqawama Lebanon

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu itaendelea kuuunga mkono mrengo wa muqawama na mapambano nchini Lebanon, mkabala wa vitisho na chokochoko tarajiwa za utawala wa Kizayuni.

Hossein Amir-Abdollahian alisema hayo jana jioni katika mahojiano na kanali ya televisheni ya Al-Manar ya Lebanon na kuongeza kuwa, Iran itaendelea kuliunga mkono na kulisaidia taifa la Lebanon kwa hali na mali.

Huku akiwapongeza wananchi wa Lebanon kwa kuundwa serikali mpya nchini humo, Amir-Abdollahian amesema Iran inauchukuliwa kwa uzito mkubwa uhuru na mamlaka ya kujitawala nchi hiyo ya Kiarabu. 

Ameeleza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu itaendelea kuliunga mkono na kulisaidia taifa la Lebanon ambalo linakabiliwa na mgogoro wa kiuchumi uliotokana na vikwazo visivyo vya kiadilifu vya Marekani.

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran ameashiria ziara yake ya hivi karibuni nchini Lebanon anayosema imeonesha uhusiano uliokita mizizi baina ya Tehran na Beirut na kubainisha kwamba, Jamhuri ya Kiislamu itaendelea kuwaunga mkono wananchi, jeshi na kambi ya muqawama katika nchi hiyo.

Wanamapambano wa Hizbullah ya Lebanon

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amegusia pia kuhusu mazungumzo yake ya kufana na Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon, Sayyid Hassan Nasrullah na kubainisha kuwa, kiongozi huyo ni shakhsia mkubwa wa kisiasa Mashariki ya Kati, na daima Jamhuri ya Kiislamu inastafidi na mitazamo yake pevu juu ya masuala ya kieneo.

Akiwa mjini Beirut, Amir-Abdollahian alikutana na kufanya mazungumzo na viongozi waandamizi wa nchi hiyo akiwemo Rais Michel Aoun, Spika wa Bunge Nabih Berri, Waziri Mkuu Najib Mikati na Waziri wa Mambo ya Nje Abdallah Bou Habib juu ya masuala ya pande mbili na ya kieneo.

 

Tags