Oct 11, 2021 11:58 UTC
  • Meli za kivita za Iran zilisindikiza meli za mafuta za Iran zilizopeleka mafuta Lebanon

Kamanda wa Kikosi cha Majini cha Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema manowari za jeshi hilo zimekuwa zikisindikiza meli za mafuta za Iran zinazopeleka mafuta Lebanon.

Admeri Shahram Irani Kamanda wa  Kikosi cha Majini cha Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameyasema hayo leo Jumatatu katika mkoa wa Bushehr kusini mwa Iran na kuongeza kuwa: "Msafara wa 78 wa Manowari za Kikosi cha Majini cha Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ukijumuisha meli mbili za kivita zilizo katika Ghuba ya Aden, umekuwa ukisindikiza meli za mafuta za Iran katika Mferezi wa Suez."

Hadi sasa Iran imetuma meli tatu za mafuta nchini Lebanon kupitia Syria ili kuisaidia nchi hiyo ambayo ilikuwa inakumbwa na uhaba mkubwa wa bidhaa hiyo.

Viongozi mbalimbali wa Lebanon wakiwemo wa kisiasa na kidini wamekuwa wakisisitiza kuwa, kutumwa meli za mafuta za Iran nchini humo kumewezesha kuvunjwa mzingiro wa Marekani dhidi ya nchi hiyo.

Admeri Shahram Irani Kamanda wa Kikosi cha Majini cha Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

Aidha Admeri Irani amesema asilimia 90 ya biashara hufanyika kwa njia ya habari na hivyo Jeshi la Majini ndio kikosi pekee cha kijeshi kinachoendesha shughuli nje ya mipaka ya Iran. Ameongeza kuwa kikosi hicho kimeweza kuwa na taathira katika diplomasia ya baharini ya mfumo mtukufu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Aidha amesema Kikosi cha Majini cha Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kina jukumu muhimu la kudumisha usalama katika njia muhimu za kiuchumi baharini na kuongeza kuwa hivi sasa hakuna tishio lolote kwa kikosi hicho. Aidha amesema kikosi hicho kiko tayari na kina uwezo wa kufika eneo lolote duniani na kinazidi kuimarisha uwezo wake.

Kamanda wa Kikosi cha Majini cha Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema leo kikosi hicho, kwa kutegemea uwezo wa ndani ya nchi kimeweza kujidhaminia zana zote zinazohitajika.

Tags