Oct 14, 2021 02:24 UTC
  • Safari ya Mkuu wa Majeshi ya Iran nchini Pakistan; mtazamo wa kimkakakati wa Tehran na Islamabad kwa ajili ya kustawisha uhusiano wa kiulinzi

Iran na Pakistan zina malengo na maslahi ya pamoja. Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana safari za pande mbili na mazungumzo ya viongozi wa nchi mbili hizo yana umuhimu wa kimkakati.

Ni kwa kutilia mkazo suala hilo, ndio maana Meja Jenerali Mohammad Bagheri, Mkuu wa Majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akiuongoza ujumbe wa ngazi za juu wa kijeshi na akiitikia mwaliko wa Jenerali Qamar Javed Bajwa, Mkuu wa Majeshi ya Pakistan, Jumanne ya juzi usiku aliwasili katika mji mkuu wa  Pakistan Islamabad katika safari yake rasmi ya siku tatu. Kustawisha uhusiano wa kiulinzi, kupanua ushirikiano wa pamoja wa mipakani, vita dhidi ya ugaidi na kujadili na kubadilishana mawazo kuhusiana na matukio ya Kanda hii na ya ulimwengu wa Kiislamu ni miongoni mwa ajenda kuu za mazungumzo ya wakuu hao wa majeshi ya Pakistan na Iran.

Katika miaka ya hivi karibuni ushirikiano wa kiulinzi na kijeshi wa Pakistan na Iran umepiga hatua kubwa na ya kuzingatiwa. Ushirikiano huo umeingia katika hatua mpya kufuatia mazungumzo ya Jenerali Qamar Javed Bajwa, Mkuu wa Majeshi ya Pakistan na Meja Jenerali Mohammad Bagheri Mkuu wa majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yaliyofanyika katika miji ya Tehran na Islamadab katika miaka ya hivi karibuni. Kwa kuzingatia umuhimu wa mazungumzo na maamuzi yaliyofikiwa katika safari na mazungumzo ya huko; kutathmini makubaliano ya kijeshi na kiusalama ya nchi mbili ni moja ya ajenda kuu za mazungumzo ya mara hii ya Meja Jenerali Mohammad Bagheri na viongozi wa kisiasa, kijeshi na kiusalama wa Pakistan.

Meja Jenerali Bagheri anatarajiwa kukutana na kufanyya mazungumzo pia na Imran Khan, Waziri Mkuu wa Pakistan na maafisa wengine wa ngazi za juu katika jeshi la nchi hiyo.

Pakistan inahesabiwa kuwa mmoja wa majirani muhimu wa Iran upande wa mashariki, na kuweko uratibu na ushirikiano baina ya nchi hizi mbili kunaweza kusaidia pakubwa kusambaratisha njama za wanaovuruga amani na usalama wa kieneo. Mshabaha na kuweko ukuruba wa kiutamaduni, kihistoria, kidini na kikaumu baina ya Iran na Pakistan sambamba na uwezo wa kiuchumi wa nchi hizi jirani, ni mambo ambayo yanalifanya suala la kustawisha uhusiano baina yao kuwa na umuhimu maradufu.

Mazungumzo ya Meja Jenerali Mohammad Bagheri, Mkuu wa Majeshi ya Iran na mwenzake wa Pakistan Jenerali Qamar Javed Bajwa

Kwa mtazamo huo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Pakistan zina fursa kubwa za kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano wa pamoja ambapo zinaweza kuwa na shughuli za pamoja katika fremu ya malengo na maslahi ya muda mrefu. Kwa muktadha huo, ndio maana kuimarishwa uhusiano na ushirikiano zaidi na mataifa ya eneo hususan majirani ni katika sera za kieneo zinazopewa kipaumbele na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran; na Pakistan ina nafasi ya kipekee katika hili.

Kuhusiana na hilo, Qasim Khan Suri, Naibu Spika wa Bunge la Pakistan ameashiria  mazungumzo yake ya hivi karibuni na kundi la ujumbe wa kirafiki wa Kibunge wa Iran na Pakistan na kubainisha kwamba, azma ya Pakistan hususan serikali ya Waziri Mkuu Imran Khan ni kustawisha zaidi uhusiano na nchi  ya Iran ambayo ni rafiki, ndugu na jirani. Iran. Pakistan na Iran zikiwa nchi wanachama amilifu katika Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC), Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi ECO na Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai zina uwezo mkubwa kwa ajili ya ushiriiano na kuwa na mitazamo mimoja kuhusiana na masuala ya eneo hili.

Fauka ya hayo, Iran na Pakistan zimekuwa zikifuatilia suala la kuimarisha ushirikiano zaidi hasa katika mikoa iliyoko katika mpaka wa nchi mbili. Katika fremu ya lengo hilo, usalama wa mpakani na ushirikiano wa pamoja, wa kieneo na matukio ya eneo hususan Afghanistan ni miongoni mwa mambo yaliyojadiliwa na pande mbili katika safari hii ya Meja Jenerali Mohammad Bagheri Mkuu wa majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Pakistan.

Ni jambno lisilo na shaka kuwa, usalama ni utangulizi wa kupanua ushirikiano wa kiuchumi wa pande mbili na eneo kwa ujumla. Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana kustawishwa uhusiano wa kiulinzi na kiusalama sambamba na kuboreshwa uhusiano wa kiuchumi ni mambo yanayopewa kipaumbele na viongozi wa Tehran na Islamabad.

Rais Ibrahim Raeisi akizungumza na Imran Khan, Waziri Mkuu wa Pakistan katika mji wa Dushanbe, Tajikistan (Septemba 2021)

Katika mazingira nyeti na hasasi ya sasa ya Asia Magharibi na kwa kuzingatia changamoto za kiusalama nchini Afghanistan na jinai za kundi la kigaidi la Daesh, kuweko ushirikiano wa kiusalama na kijeshi baina ya Tehran na Islamabad kuna ujumbe maalumu. Kwa mtazamo wa viongozi wa nchi mbili ni kuwa, kuimarishwa uhusiano na ushirikiano wa kiulinzi na kiusalama sambamba na uhusiano wa kisiasa na kiuchhumi ni jambo lenye umuhimu wa kimkakati.

Matukio machungu ya kigaidi katika mipaka ya pamoja na katikka uga wa kieneo ni ithibati tosha kwamba, kung'oa mizizi ya ugaidi kunahitajika ushirikiano wa dhati na wa kweli baina ya nchi za Ukanda huu. Safari ya Meja Jenerali Mohammad Bagheri Mkuu wa Majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Pakistan na mazungumzo yake na viongozi mbalimbali wa Islamabad kiuhakika ni jibu la mahitaji haya.